Na Gift Mongi
Moshi
Kwa ajili ya kuweza kuwasaidia vijana na tafsiri sahihi ya neno kijana mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi(UVCCM)wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro Yuvenail Shirima mapema hii leo june 12.2023 ameendeasha darasa huru kuhusu wajibu wa kijana na maana yake kiujumla.
Amesema neno kijana limekuwa na maana pana sana na kutolewa tafsiri mbalimbali kwa kuzingatia jamii husika au yaifa Fulani.
'Mfano nchini Tanzania ni mtu mwenye miaka 18-35[45], yaani baada ya balehe na mabadiliko ya kimaumbile toka utotoni kuelekea ukubwani.'amesema
Aidha kwa mujibu wa sera ya taifa ya maendeleo na vijana ya mwaka 1996 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2007, inasemekana kijana ni mtu mwenye umri kuanzia 15-24[45] kwa mantiki hiyo basi kijana ni mtu yoyote wa kike au wa kiume mwenye umri kuanzia miaka 18-35[45], ambaye kwa mujibu wa mifumo ya kijamii au kitamaduni ,kisiasa na kisheria ana uwezo wa kujitegemea na kujiamulia kufanya maamuzi yake binafsi.
Amesema kuwa kijana ni mtu muhimu sana kwa taifa lolote lile kwani ndio nguvu kazi ya taifa, ndio taifa la kesho, ndio tumaini la taifa ndio mtu anayetazamiwa kwa mapana ya nchi.
'Jamani tuseme ukweli kuwa vijana hawa wanakumbana na changamoto mbalimbali katika maisha yao ya ujana na mwisho wa siku taifa linamchukulia kijana kama mtu aliyeshindwa tayari na asiye na msaada wowote kwa taifa lake kitu ambacho sio sawa'anasema
Ameongeza kuwa katika umri huu wa ujana inampasa kijana kujitambua ili aweze kuwa na muonekano halisi wa kijana sio kwa umri tu bali matendo zaidi.
Kwa mujibu wa Shirima ni kuwa yapo mambo kadhaa ambayo yanabeba dhana mzima ya kijana kama ifuatavyo
Kijana ni lazima awe na utambuzi binafsi {personal recognition}, utambuzi wa jamii yake na mazingira yanayomzunguka. Kujitambua kunamfanya kijana kufanya mambo sahihi na kuenenda sawa na maadili ya jamii na taifa kwa ujumla.
Hivyo basi kijana sio idadi ya namba tu bali kijana ni zaidi ya namba za umri ulizonazo kwa kujitambua wewe mwenyewe kwanza na kutambua mazingira yanayokuzunguka.
Na anasema kijana yoyote wakitanzania anapaswa kujitambua hii ni silaa kubwa sana katika maisha ya ujana.
MAAMUZI.
Maamuzi ni chaguo analofanya mtu, chaguo hili linaweza kuwa sahihi au lisiwe sahihi. Lakini maamuzi ni matokeo ya mawazo ya kitu Fulani.
Hivyo basi hatua yoyote ya maamuzi kwa kijana kwenye maisha yake, huweza kuleta matokeo sahihi au yasiyo sahihi.
Kijana ni muhimu kuwa mtu wa tofauti na kufanya maamuzi sahihi kwani maamuzi unayoweza kufanya leo yanaweza kukusaidia na kufanya maisha yako kuwa mazuri au kuharibu ujana wako na maisha yako kwa ujumla.
Maamuzi ni sumaku inayovuta kutenda mabaya au mazuri, kama kijana chagua kutenda mema kwani kesho yako huwa halisi unapofanya maamuzi sahihi leo.
UWELEWA WA CHANGAMOTO
Ni lazima kijana aelewe changamoto mbalimbali na kujua jinsi ya kukabiliana nazo, kwani changamoto huwa hazikimbiwi ila tuna zitatua au kuzipunguza kwa namna salama.
Kumekuwa na vijana ambao huchukulia ugumu wa changamoto hizi kutenda mambo mabaya kama kujiingiza katika vikundi vya kigaidi, uvutaji bangi na madawa ya kulevya kwa ujumla.
Kama kijana halisi na anayejitambua atachagua njia salama za kutatua na kukabilana na changamoto. Matatizo haya au changamoto ni kama ukosefu wa ajira kwa vijana wengi hasa pale wanapomaliza elimu zao, kukosa elimu ya stadi za maisha, elimu ya afya nk.
KUJENGA HOJA.
Umri mzuri wa kuwa na hoja na zenye nguvu katika masuala mbalimbali ni kijana.
Ni lazima uwe mwepesi kushiriki masuala mbalimbali ya kujenga hoja hasa zenye maslahi mapana kwa jamii inayokuzunguka au taifa kwa ujumla.
Kujenga hoja, kutetea na kupinga hoja zisizo na mashiko kwa vijana wa kitanzania kwa kufanya hivi kijana anajenga nafasi nzuri ya kusikilizwa na jamii lakini pia kuaminiwa kwa ushawishi wa hoja katika umri wako wa ujana.
USHAWISHI.
Kijana ni lazima awe na ushawishi katika masuala muhimu na kwa manufaa ya jamii kwa ujumla hasa kwa vijana wenzake, katika kushawishi ndio tunaona nguvu ya kijana na kuanza kutengeneza taifa imara.
Vijana wengi kwa sasa tunajitahidi sana kuwa na nguvu ya ushawishi, pia tunaona asasi nyingi zikiongozwa na vijana wenyewe ili kuweza kushawishi mambo yenye tija kwa maisha ya vijana.
Lakini pia hata serikalini vijana wengi wameaminiwa na kuoesha ushawishi mkubwa sana kuwa wana uwezo wa kufanya kazi na hivyo kuaminiwa na serikali.
UKOMAVU WA AKILI.
Kuwa na akili ya kufanya mambo yanayoendana na umri wako. Vijana wa kitanzania ni lazima waendane sawa na umri wao hii itasababisha hata kufanya mambo makubwa zaidi katika jamii na yenye matokeo chanya, wawe na uwezo wa kumshauri kijana au vijana wenzao, familia au jamii husika kwa kutoa dira kwa vijana wenzao, hii itaambatana na kupanga mipango na kuanza ufuatiliaji ili mipango itimie kama vile kubuni wazo fulani lenye lengo/manufaa kwa kijana au kwa jamii, biashara au kufikiria kazi nzuri anayoweza kufanya.
KIJANA LAZIMA ATAMBUE MAMBO HAYA;
AJITAMBUE.
Kijana lazima ajitambue na kutambua fursa mbalimbali zinazomuhusu,
Unapojitambua ni lazima ujue thamani yako na kusudi la uwepo wako, kwa kujitambua unaweza kufanya mambo mazuri sana kwa jamii na taifa kwa ujumla.
AJIKUBALI
Kujikubali ni hali ya kupokea mambo yote yanayokuhusu, kijana anapaswa kujikubali jinsi alivyo hii itamsaidia kusonga mbele Zaidi. Mfano mtu una tatizo fulani na ambalo linakufanya tofauti na wengine unapaswa kujikubali, ili ujione kuwa ni wa thamani kama wengine walivyo.
Kwani unapojikubali unaweza kujiona wa kawaida na kufanya mambo makubwa kwa familia,jamii na taifa kwa ujumla, na kufanya utambulike na unaweza kuwa mfano wa kuigwa.
AWE NA SHAUKU,NIA NA KIU.
Kijana ni lazima awe na awe na shauku nia na kiu ya kufanya vitu tofauti tofauti venye lengo la kuelimisha au kutimiza kusudi, maono au matarajio yao.
AWE MZALENDO.
Kijana anapaswa kuwa mzalendo sana, hapa kama kijana inabidi ujiulize na kujua kusudi la kuwepo Tanzania.
Ni lazima ujue unapaswa kuwa mzalendo kwa nchi yako. Ufanye yaliyo mazuri kwa nchi yako, ufanye yaliyo mazuri kwa jamii yako ya kitanzania.
MAMBO YANAYOMBEBA KIJANA
NIDHAMU.
Nidhamu ni uwezo wa kufanya mambo/vitu fulani pasipo kufuata hisia[ kinyume na ulivyozoea]. Kijana/ujana ni lazima uambatane na nidhamu ya hali ya juu ili aweze kuvuka vikwazo mbalimbali.
HESHIMA.
Ni hali ya ndani ya uthamani anaokuwa nao mtu kwake na mwingine au ujali wa kuangalia rika kujenga uthamani na hii tunaweza kusema ni asili ila jamii wanaijenga au wazazi wanaijenga ili ushirikiano uwepo.
Hivyo basi heshima utakayoionesha wakati wa ujana wako ndio itakayokusaidia/kukubeba katika maisha yako ya ujana mpaka uzeeni.
UWAJIBIKAJI.
Ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa.
Hivyo basi jifunze kuwajibika katika majukumu mbalimbali ili ufanikiwe, msingi wa maisha yako ni lazima kufahamu namna ya kujiandaa na maisha yako ya baadaye.
Uwajibikaji katika uongozi hadi maisha ni moja ya misingi na nguzo mama inayotubeba kama kijana, kwani uwajibikaji bora huleta matokeo chanya kwenye kila wazo,mpango au maono fulani.
UADILIFU.
Ni hali ya kuwa mwaminifu na kuwa na mwenendo mzuri katika utendaji kazi au kitu chochote kile.
Uadilifu unahusisha kujali watu, kujali muda, kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na kuwa mkweli.
Haya ni mambo ya msingi ambayo kijana anapaswa kujua lakini pia kuishi katika hali hii, kwani utajikuta ukiwa kijana wa thamani katika jamii yako lakini pia taifa kwa ujumla.
0 Comments