Mjumbe huyo wa NEC amesema, tayari Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan ameshanyoosha njia ya kuifanya CCM ishinde, kwa kuwa ndani ya miaka miwili ya Uongozi wake, Serikali imetekeleza miradi mingi ya maendeleo, na mingine ipo katika hatua za utekelezaji.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamoud Abou Jumaa, akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM katika mkutano uliofanyika Mlandizi, akiwa katika ziara ya kuimarisha Chama na kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Chama wilaya ya Kibaha Vijijini mkoa wa Pwani, jana.
Alisema kwa hali ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ni nzuri kwa kuwa kwa upande wa shule vyumba vya madarasa vinajengwa kila Kona, huduma za afya zahanati na vifaa tiba vimesambazwa kila kijiji na vituo vya afya ambapo Sasa huduma hata za upasuaji hutolewa hadi vijijini.
Alisema, kuwepo kwa wanachama hai na mshikamano ndiyo njia pekee ya uhakika itakayoweza kukifanya Chama kishinde katika Uchaguzi unaokuja wa Serikali za mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, na kusisitiza kuwa hayo ni lazima yafanyike kwa kuwa lazima CCM ishinde katika chaguzi hizo.
Hatahivyo Hamoud alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) Makao Makuu kimesema hakivitambui vikundi vinavyojiita 'Chawa' na kwamba vikundi hivyo havina baraka ya Chama, hivyo wale wote wanaokipenda chama waunde vikundi vyenye faida vya ujasiriamali.
" Kuna jambo moja linaendelea endelea la Chawa, Chawa, likiihusisha CCM, na uzuri baadhi ya viongozi wa Chama mpo hapa, hili neno linatambatambaa sana, sasa CCM Makao makao makuu tunasema hilo Chawa chawa halina baraka za CCM".
Hivi vikundi cha chawa unaweza ukaanzisha iwe Chawa, nyuki, panzi au mdudu yeyote hatukatai, lakini siyo kwa faida ya CCM, cha msingi ni kuunda vikundi vyenye faida vya ujasiriamali", alisema Mjumbe huyo wa NEC. na kuongeza kuwa ametoa tamko hilo kwa nafasi yake ya Mjumbe wa NEC kwa kuwa ni maelekezo ndani ya Chama ngazi ya taifa.
Akizungumzia Uhai wa Chama Mjumbe huyo wa NEC, aliwataka viongozi na wanachama wa CCM njia ya kwanza ya kuimarisha uhai wa CCM na Jumuiya zake ni kuhakikisha kunakuwepo wanachama hai na kinachofuata ni mshikamano wa viongozi na wanachama kufanya kazi kwa umoja na mshikamano wa dhati.
Katika ziara hiyo Wilaya ya Kibaha Vijijini, Mjumbe huyo wa NEC alikagua utekelezaji wa ilani ya CCM kwa utembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Ofisi za CCM Matawi ya Saidi Domo na Mkwani, Zahanati ya Vikuruti, Mradi wa Zahanati Ruvu Maji na eneo la Viwanda.
Baada ya kutoka Kibaya Vijijini mkoa wa Pwani jana, leo Mjumbe huyo wa NEC anaendelea na ziara hyo ya Kitaiafa katika mkoa wa Dar es Salaam.
0 Comments