Header Ads Widget

NEEMA YAJA KWA WANANCHI WA URU KUSINI JIMBO LA MOSHI VIJIJINI.

 


NA WILLIUM PAUL.

SERIKALI kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi imeahidi katika mwaka mpya wa fedha 2023/2024 wanampango wa kununua vifaa tiba ambapo baadhi vitapelekwa katika kituo cha Afya Uru kusini katika Jimbo la Moshi vijijini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro ili wananchi wapate huduma.


Hayo yamekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof Patrick Ndakidemi kuuliza swali la nyongeza Bungeni ambapo aliishukuru Serikali kwa kujenga kituo cha Afya Uru kusini na karibu kitakamilika ujenzi wake je Serikali inampango gani kupeleka vifaa tiba na wataalam wa Afya katika kituo hicho ili wananchi waanze kupata huduma.


Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Deogatius Ndejembi alisema kuwa, Serikali katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 imeajiri watumishi wa Afya wapatao 8000 hivyo wengine watapangiwa katika Halmashauri ya Moshi ambapo wataenda katika kituo hicho cha Afya.


Naibu Waziri, Ndejembi alisema kuwa, pia katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kununua vifaa tiba ambapo watahakikisha vifaa vingine vitaenda katika Jimbo la Moshi vijijini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi ikiwamo kituo cha Afya cha Uru kusini.


Kupatikana  kwa vifaa pamoja na wataalam kutasaidia kituo hicho cha Afya Uru kusini kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa kata ya Uru kusini, Uru kaskazini na kata za jirani ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kupata huduma za Afya.


"Wakinamama wajawazito, wazee wamekuwa wakiteseka sana kutembea umbali mrefu kupata huduma za Afya hivyo kuanza kutolewa huduma katika kituo chetu hichi kitatusaidia kupunguza gharama na mwendo tuliokuwa tukiutumia kwenda kupata huduma za Afya" alisema Neema Macha.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI