Header Ads Widget

BARABARA YA GETIFONGA-MABOGINI - KAHE KWA KIWANGO CHA LAMI KUIGHARIMU SERIKALI BILIONI 28.59.



NA WILLIUM PAUL.

WANANCHI wanaoishi katika maeneo ya Mabogini na Kahe katika Jimbo la Moshi vijijini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wanaenda kuondokana na adha ya barabara baada ya Serikali kuanza kutenga fedha za ujenzi wa barabara ya Getifonga- Mabogini- Kahe kwa kiwango cha lami.


Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof Patrick Ndakidemi kuhoji Bungeni je ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Getifonga- Mabogini- Kahe.


Aidha Mbunge huyo aliishukuru Serikali kwa kutenga milioni 475 kutengeneza barabara ya TPC- Samanga-Chemchem lakini tamanio la wananchi lilikuwa ni kutengeneza daraja mto Ronga linalounganisha vijiji vya Samanga na Chemechemi.


Je Serikali inampango gani kutengeneza daraja hilo huku pia akihoji barabara ya International School- Kibosho KNCU- Kwa rafaeli haijakamilika kwa kiwango cha lami je Serikali inampango gani wa kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.


Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri, OR-Tamisemi, Deogratius Ndejembi alisema kuwa, barabara ya Getifonga-Mabogini-Kahe ipo kwenye Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 kuijenga kwa kiwango cha lami.


Ndejembi alisema kuwa, hadi sasa Tarura mkoa wa Kilimanjaro wamekamilisha usanifu wa kiwango cha lami ambapo inahitajika Bilioni 28.59 ili kujengwa.


Alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Tarura ilitenga Milioni 158.85 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya urefu wa kilomita 12 na kazi imeshakamilika.


Naibu Waziri huyo alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 1.2.


"Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami" alisema Naibu Waziri Ndejembi.


Alisema kuwa, kuhusu barabara ya Samanga- Chemchem kuhitaji daraja ni kweli Serikali ilitenga milioni 475 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo hivyo wataangalia katika bajeti ya mwaka 2023/2024 ya Tarura kuona imetenga kiasi gani kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.


Aliongeza kuwa, watamuelekeza Meneja wa Tarura mkoa wa Kilimanjaro kuweza kuelekea fedha mara moja kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.


Kuhusu barabara ya International School-Kibosho KNCU-Kwa rafaeli alisema kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara hiyo kadiri upatikanaji wa fedha.


"Tutaangalia katika bajeti ya fedha ya mwaka 2023/2024 ni namna gani tutaweza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ya International School-Kibosho KNCU-Kwa rafaeli kwa kiwango cha lami" alisema Naibu Waziri Ndejembi..


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS