Header Ads Widget

UMMY MWALIM MGENI RASMI MAADHIMISHO YA FISTULA KIGOMA



Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa maadhimisho ya siku ya Fistula yatafanyika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Mei 23 mwaka huu ambapo Waziri wa afya Ummy Mwalim anatarajia kuwa mgeni rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma Andengenye alisema kuwa maadhimisho hayo yanakuja mkoani Kigoma wakati mkoa huo ukishika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuwa na idadi ya wagonjwa wengi wenye Fistula.


Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa bado matibabu ya Fistula kwa mkoa Kigoma yamekuwa magumu kutokana na wagonjwa wengi kutokuwa na taarifa sahihi juu ya ugonjwa huo na hivyo wagonjwa wengine hukimbilia kwa waganga wa kienyeji kupata matibabu na kwamba maadhimisho haya ya Kitaifa yatakuwa mwanzo wa mkakati wa mkoa kukabiliana na hali hiyo.


Akieleza kuhusu maadhimisho hayo Mratibu wa afya ya mama na mtoto kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Bernadeta Peter alisema kuwa imani za kishirikiana kuhusu wanawake wanaopatwa na ugonjwa wa fistula kwamba unatokana na kurogwa umechangia wanawake hao kujificha na kushindwa kupata matibabu yanayostahili.



Bernadeta alisema kuwa mkoa Kigoma na moja ya mikoa inayoongoza kwa idadi kubwa ya wanawake wanaoupata matatizo ya Fistula ukishika

nafasi ya tatu lakini bado idadi kubwa ya wanaopata matatizo hayo hawajitokezi kupata matibabu kwa imani kwamba matatizo hayo yanatokana na imani za kishirikina.

 

Sambamba na hilo alisema kuwa wanawake wengi wanajificha na kushindwa kupata matibabu mapema kwa kuogopa unyanyapaa kulingana na hali yao ya kutokwa na haja ndogo wakati wote lakini kuogopa maneno ya mtaani kuwa wanawake wanaopata Fistula wanatokana na kufanya mapenzi na wanaume wengi.

Kutokana na hilo alisema kuwa wamepanga kutumia wiki ya maadhimisho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matatizo ya ugonjwa huo na namna wanavyoweza kuzuia ikiwemo wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki ili kuweza kushughulikia matatizo yanayojitokeza kabla ya kujifungua na kwamba wiki hii kwa kushirikiana na CCBRT wanatoa huduma za upasuaji bure.


Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dk.Ibrahim Salehe alisema kuwa pamoja na mkoa Kigoma kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaoathirika na Fistula lakini wengi wanakimbilia hospitali ya CCBRT bila kuanzia hospitali yeyote ya mkoa pamoja na kwamba mkoani humo vipo vituo viwili vinavyotoa huduma ikiwemo operesheni kwa wagonjwa.


Alisema kuwa kwa wiki hii ya maadhimisho ipo kambi maalum ambayo itatoa matibabu ambayo yatatolewa bure na madaktari bingwa wa mkoa huo wakishirikiana na wale wa CCBRT ambapo ametoa wito wanawake wote walioathirika kujitokeza kupata matibabu.

 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI