Header Ads Widget

MBOWE - CHADEMA INARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MARIDHIANO

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma


CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kuanza kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani ni matokeo ya maridhiano ya dhati yaliyoanzishwa baina ya viongozi wa CHADEMA  na CCM chini ya  serikali ya Raisi Samia Suluhu Hassan.


Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema hayo kwenye viwanja vya Mwanga Centre Mjini Kigoma katika uzinduzi wa mpango wa chama hicho wa operesheni  katiba mpya unaojulikama kama +255.



Mbowe alisema kuwa kwa miaka saba vyama vya upinzani havikuwa na nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara wala mahali pa kusemea  kuwaambia wananchi ni kwamba jambo hilo liliwafanya kuwa kama wamekabwa koo na sasa wanapumua.


Mwenyekiti huyo alisema kuwa moja ya viashiria vya maridhiano kutekelezwa kwa vitendo ni kitendo cha maandamano ya BAWACHA kwenda ofisi ndogo za bunge Jijini Dar es Salaam kupinga uwepo wa wabunge wa kuteuliwa na Msajili wa vyama vya siasa kutoka CHADEMA ambao hawakuwa na ridhaa ya chama hicho ambapo maandamano hayo  yalisindikizwa na polisi badala ya kupigwa virungu.


" tunaridhika na hatua ya maridhiiano ambayo imeanza kutekelezwa lakini hatutaki iishie hapa na kwa sababu mwanzo umekuwa mzuri tunaomba hili lifanyike hadi tutakapoelekea kwenye uchaguzi mkuu"Alisema Mbowe.


Akizungumzia operesheni Katiba Mpya alisema kuwa kwa miezi miwili viongozi wakuu wa chama hicho watakuwa kwenye mikoa ya kanda ya Magharibi ambayo ni Kigoma,Katavi na Tabora kuelimisha wananchi kuunga mkono mpango wa mabadiliko ya Katiba mpya kuelekea kupata tume huru ya uchaguzi.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA,Tundu Lisu aliwataka wananchi wa mkoa Kigoma kuunga mkono mabadiliko ya Katiba ili kupata katiba mpya kwani katiba ya sasa imekuwa na matatizo mengi ikiwemo ya masuala ya uraia ambayo wananchi wa mkoa Kigoma ni Wahanga.


Lisu alisema kuwa changamoto ya Katiba ya sasa haizungumzii uraia wa Mtanzania hivyo ni lazima kuleta katiba ambayo itakuwa sehemu ya maisha ya wananchi wake kwani pale wananchi wanapopingana na mawazo ya serikaki katiba inawashughulikia ikiwemo masuala ya uraia.


Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu CHADEMA  Zanzibar, Salum Mwalimu alisema kuwa atakuwa mtu wa mwisho kupinga uwepo wa muungano kwani muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar una faida kubwa kwa wananchi wa pande zote.


Hata hivyo Mwalimu aliswma kuwa muungano umekuwa na changamoto mbalimbali za kikatiba hivyo mabadiliko ya katiba hayana budi kufanyika ili kuufanya muungano huo kuwa imara na wananchi kufaidi matunda ya muungano.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI