Header Ads Widget

TUWAJALI KWA VITENDO WATU WENYE ULEMAVU - MHE. OTHMAN

 



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ametoa wito kwa Viongozi wa Tawala za Mikoa kutekeleza kwa vitendo Sera na Sheria Mpya kwaajili ya Watu Wenye Ulemavu Nchini, ili kufanikisha juhudi za Serikali katika kuwahudumia wananchi wake.  


Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akifungua Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, na Makamanda wa Polisi kutoka Mikoa yote ya Unguja na Pemba, huko Hoteli ya Madinatul-Bahr, Mbweni Zanzibar.


Amesema ni wajibu kwa Viongozi na Watendaji hao kutambua kwamba kunahitajika kuanzishwa Mabaraza ya Wilaya ya Watu Wenye Ulemavu, kwa mujibu wa Sheria Nambari Nane (8) ya Mwaka 2022, kupitia Kifungu cha 16 hadi 19, sambamba na kuwashajiisha Masheha waliomo katika Wilaya zote kuwabaini, kuwafichua na kuwasajili watu wenye ulemavu, wanaoishi ndani ya Shehia zao.


Mheshimiwa Othman amewanasihi Wakuu wa Wilaya pamoja na Vyombo vya Dola kuyasimamia kikamilifu  Mabaraza hayo ili kufikia Malengo na Matarajio ya Serikali, katika kuwahudumia na kuwatendea haki wananchi wote, bila ya kuitenga sehemu hiyo muhimu ya Jamii ya Watu Wenye Ulemavu.


”Napenda kutoa wito kwenu, kuwa Mabalozi wema wa kuyapokea, kuyafikisha na kuyatendea kazi Mafunzo haya muhimu, pamoja na kuhakikisha tunawapenda na kuwajali watu wenye ulemavu; tukawe mfano wa kukemea na kuachana na tabia zote za kuwadhalilisha, ikiwemo kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwaita majina yasiyofaa, tukiamini pia kwamba sote ni viumbe wenye haki, huku kila mmoja akiamini naye ni mlemavu mtarajiwa”, amesisitiza Mheshimiwa Othman.


Aidha, Mheshimiwa Othman ameongeza kusema, ”pamoja na hatua na jitihada za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwalinda na kuwajali watu wenye ulemavu, bado sehemu hiyo muhimu ya jamii inaendelea kuzungukwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kutengwa, kubaguliwa, kubughudhiwa na hata kutendewa kila aina ya ukatili.


Hivyo, licha ya kuhimiza mashirikiano ya Viongozi na Watendaji hao katika kupambana na changamoto hizo, Mheshimiwa Othman ameshukuru pia juhudi zinazochukuliwa na Wahisani pamoja na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Nchi, akisema kuwa jitihada hizo zinadhihirisha kwamba wanajali maendeleo ya watu wenye ulemavu, na ustawi bora wa jamii kwa ujumla.



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Harusi Said Suleiman, ameshukuru jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na Jumuia mbalimbali za Watu Wenye Ulemavu, zikiwemo za Kutungwa kwa Sera ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2008; na Sheria Mpya ya Watu Wenye Ulemavu Nambari 8 ya Mwaka 2022, kwa azma ya kuilinda sehemu hiyo muhimu ya jamii.


Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dokta Omar Dadi Shajak, amebainisha mafanikio makubwa kupitia Mfululizo wa Mafunzo hayo hapa Visiwani akisema, tayari wameshawafikia Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Taasisi za Umma, wakiwemo Makatibu wa Kamati zote za Kudumu za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Maafisa Wadhamini, Makatibu na Manaibu Katibu wa Wizara zote za Serikali.


Kabla ya kuwakaribisha Viongozi hao kuhutubia Hafla hiyo, Mkurugenzi wa MECP-Z, Bi Sharifa Majid amefahamisha kuwa Taasisi yake, iliyopo chini ya Shirika la Aghakhan (Aghakhan Foundation) iliyoasisiwa takriban miaka 40 iliyopita, imeweza kufanikisha juhudi mbali mbali za kuiungamkono Serikali, Jamii, sambamba na uandaaji wa Mafunzo hayo, tangu walipoasisi Mradi wa Moja kwa Moja kwaajili ya Watu Wenye Ulemavu, mnamo Mwaka 2019.


Mafunzo hayo ya Siku Moja ambayo yameandaliwa na Taasisi ya ’Madrassa Early Childhood Program Zanzibar’ (MECP-Z) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, pamoja na Ufadhili kutoka Serikali ya Norway, yanalenga katika kujenga uelewa wa masuala ya watu wenye ulemavu ili kuyazingatia katika mipango mbalimbali ya maeneo ya kazi yakiwemo ya Majengo, utekelezaji wa Mwongozo wa Miundombinu Rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu uliotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; kuweka mikakati ya kuwafichua na kuwatambua watu wenye ulemavu waliomo katika Shehia mbalimbali sambamba na mahitaji yao; na kuwazingatia watu wenye ulemavu katika utoaji wa huduma zote za kijamii.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI