Mwanaume mmoja mkazi wa kitongoji cha Darajani kijiji cha Malolo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro alitajwa kwa jina la Aman Malekela (72) amejiua kwa kujichoma moto ndani ya chumba chake yeye na watoto wake watatu kwa kile kinachodaiwa ni msongo wa mawazo kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsibu pamoja na ugumu wa maisha .
Wakizungumza Leo na mwandishi wa Matukio Daima Media aliyefika eneo la majirani wa marehemu huyo walisema kuwa siku zote enzi za uhai wake marehemu alikuwa akilalamika hali duni ya maisha kiasi cha kushindwa kupata fedha ya matibabu ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
Alisema mmoja kati ya majirani wa marehemu huyo Aman Alli kuwa siku moja kabla ya kifo chake walikutana na kubwa alikuwa akilalamika kukosa fedha za mahitaji ya nyumbani pamoja na fedha za matibabu za ugonjwa ambao alidai ulikuwa ukimsumbua (bila kutaja ugonjwa huo) alisema ni muda mrefu amekuwa akiumwa na akijiuguza mwenyewe .
Hata hivyo alisema taarifa ya tukio la kifo cha mzee huyo na watoto wake alikipata kwa majirani na baada ya kufika katika nyumba yake walishuhudia moto mkubwa ukiendelea kuwaka ndani ya chumba chao kabla ya wananchi kuchukua hatua ya kuzima moto huo ambao hata hivyo tayari uklikuwa umekwisha sababisha vifo vya mzee huyo na watoto wake watatu .
Angela Malekela Madunda ni mjukuu wa mzee huyo ambae ni mhanga wa tukio hilo alisema kuwa juzi majira ya saa 3 usiku baada ya kurejea nyumbani hapo alikuta mzee wake huyo akiwa ametoa chumbani kwake sebuleni cherehani na vitu vingine vya thamani na baada ya kumuuliza sababu ya kuvitoa vitu hivyo ndani alimjibu kuwa amefanya hivyo kwa usalama wa vitu hivyo .
" Sikujua kama babu anataka kufanya maamuzi mazito ya kujiua na watoto wake ndani maana baada ya kutoa vitu hivyo aliwaita watoto hao watatu na kuingia nao ndani kulala kitanda kimoja na usiku muda kama wa saa 7 usiku hivi mimi nikiwa nimelala chumba cha pili nilishtushwa na joto kali ndani ya nyumba pamoja na moshi mzito uliokuwa ukitoka chumbani kwa babu" alisema binti huyo mwenye miaka kati ya 27 .
Kuwa yeye alikuwa amelala na mtoto wake chumbani na baada ya kuona hali hiyo ya moto alitoka nje na mtoto na kuanza kupiga kelelea kuomba msaada kwa majirani ambao walifika na kuanza kuzima moto huo .
Alisema kwa kawaida watoto hao watatu huwa wanalala kwa zamu kwa mama yao aliyepo ng'ambo ya pili ya daraja kwa maana ya wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa na baba yao ambae yupo upande wa Kilosa na siku hiyo ya tukio walikuja kulala kwa baba yao kama kawaida .
Kuwa mzee huyo alitengana na mke wake na hivyo siku zote amekuwa akiishi mwenyewe na yeye kama mjukuu na watoto hao ambao wamekuwa wakija kwa zamu kulala na baba yao.
Hata hivyo alisema nyumba hiyo haikuwa na umeme wala ndani hakukuwa na kibatali ,taa wala aina yoyote ya moto na anashangazwa na chanzo cha moto huo usiojulikana ambao wamepelekea vifo vya ndugu zake ni wapi umetokea.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Sufian Ramadhan alisema kuwa wao kama serikali ya kijiji baada ya kupata taarifa ya moto huo walikimbia kituo cha Polisi Ruaha Mbuyuni kutoa taarifa na polisi walipofika walikuta tayari vifo hivyo vimetokea .
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Morogoro Alex Mkama alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo .
Kamanda Mkama alisema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha vifo hivyo ni moto ambao uliwashwa ndani ya chumba hicho baada ya maandalizi yote ya moto huo kufanywa na mzee huyo .
Kwani alisema wamebaini kuwa kabla ya kujiteketeza kwa moto marehemu na watoto wake walijifungia ndani ya chumba hicho na kuwa marehemu alikuwa mnufaika wa mradi wa TASAF .
Aliwataja waliofariki dunia kwa moto huo kuwa ni Aman Malekela Madumba (72) ambae ni baba wa watoto hao pamoja na watoto wake Habibu Madumba (10), Sadiki Madumba (8) na Bahath Madumba (5) ambao wote walikuwa ni wanafunzi wa shule ya msingi .
0 Comments