Header Ads Widget

KAMATI ZA ULINZI WA WATOTO NA WANAWAKE WATAKIWA KUZINGATIA MWONGOZO WA UANZISHWAJI WA KAMATI HIZO

 



 WMJJWM, Dar Es Salaam


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameziagiza Kamati za Ulinzi wa Watoto na Wanawake ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia Mwongozo wa Uanzishwaji wa Kamati hizo ili kuepusha matukio ya Ukatili hasa kwa Watoto yanayopelekea vifo na majonzi katika jamii.


Hayo yamejiri leo Aprili 26, 2023 katika mkutano wa Waziri Dkt. Gwajima na Wananchi wa Mtaa wa Ngwale, Kata ya Chanika alipowatembelea kuwapa pole kufuatia tukio la watoto wawili kuuawa usiku wa kuamkia tarehe 24 Aprili, 2023 na baba yao mzazi kwa kile kinachodaiwa ugomvi na mwenzi wake.


Aidha, ameelekeza kuundwa kwa Madawati ya Ulinzi wa Watoto Shuleni katika Shule zote za Kata ya Chanika na lifanyike tamasha kubwa la kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto kufuatia tukio hili la kusikitisha.



Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa maendeleo na ustawi wa nchi ikiwemo mifumo ya kuwafikia wananchi hadi ngazi ya chini.


"Kata hii ina Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Viongozi wa Dini, Polisi, wadau wengine .

Mifumo ikifanya kazi vizuri itaepusha mambo mengi lakini pia kamati  zinahitaji ushirikiano na lazima tujenge mazingira ya kuepusha mambo haya katika jamii la si hivyo matukio kama haya yataendelea" amesema Dkt. Gwajima.


Amesema kama jamii ina uwezo wa kufanya mambo makubwa bila kusubiri miongozo ya Serikali kama harusi zilizopangiliwa kwa ufanisi, maana yake wananchi wana akili na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii zinazojitokeza kwenye maeneo yao.



Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kufika haraka na kuchukua hatua

kwa mtuhumiwa kwani matukio mengi yamekuwa yakiyokea katika jamii hivyo kama wadau na jamii itashirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa itasaidia kupambana na matukio ya ukatili .


Akisimulia mkasa huo Mwenyekiti wa Mtaa wa Ngwale Bajari Matimbu na Kaka wa mtuhumiwa wa mauaji hayo wamesema mtuhumiwa aliwanywesha sumu watoto wake na yeye kutaka kujiua kwa kujitumbukiza kwenye shimo ambapo aliokolewa.



Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar Es Salaam Elisha Nyamara amesema Wilaya ya Ilala hasa Chanika na Tabata bado kuna matukio ya ukatili hasa kwa Wanawake na Watoto ambayo ni changamoto kwa ustawi wa jamii. 


Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Afisa Tawala Flora Mgonja, ameendelea kukemea tabia ya watu kujiamulia mambo wakati vyombo husika vipo hivyo wanatakiwa kutoa taarifa ili waweze kupata msaada zaidi.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI