Header Ads Widget

WAPEWA BOTI 12 ZA UVUVI WAWEZE KUJIAJIRI

 



Na Fadhili Abdallah,Kigoma


Shirika la Africa Relief Organization la nchini Kuwait lenye tawi lake nchini Tanzania limekabidhi boti  12 za kuvulia samaki , nyavu  12 pamoja na mashine  12  kwa wavuvi wa manispaa ya Kigoma Ujiji wanaofanya shughuli zao kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika ili kuwawezesha kuwa na shughuli ya kujiingizia kipato.


Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 70 vilikabidhiwa kwa Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye kwa niaba ya wavuvi hao na Mkurugenzi wa shirika hilo nchini, Dk Sammy Aazib ambaye alisema kuwa ugawaji wa vyombo hivyo vya uvuvi ni moja kati ya miradi yao ya kimkakati ya kunyanyua hali za kiuchumi za wananchi na kwamba vifaa hivyo  vimetolewa kama ruzuku.


Mkurugenzi huyo alisema kuwa kutolewa kwa vifaa hivyo kama sadaka ni kutekeleza maagizo ya Mtume Muhamad (SAW) ambaye anafundisha kuwa mtu bora ni Yule ambaye anahangaika kutafuta riziki yake ya siku kwa jasho badala ya kupita mitaani na kuomba omba hivyo misaada hiyo imelenge kuwatengenezea ajira watu mbalimbali ambao hawana shughuli za kufanya.


Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Wavuvi hao Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka wavuvi wanaofanya shughuli zao katika  ziwa Tanganyika mkoani Kigoma kutojihusisha na uvuvi haramu unaohusisha upigaji wa baruti, vyavu zilizopigwa marufuku katika shughuli za uvuvi kwani matumizi ya vitu hivyo  yanaharibu mazingira ya ukuaji wa samaki katika ziwa hilo.




 “Niombe sana tutunze mazingira yetu tunapoenda kuvua samaki, kama tusipoyatunza tutazunguka na vivyo vyombo vya kuvulia na mtarudi bila samaki, ili tuendelee kwenda kuvua na kurudi na samaki lazima tutunze mazingira, samaki wanahitaji mazingira yaliyotunzwa ili waweze kuzaliana na kukua na ndipo tuweze kuwavua,”alisema Andengenye.



Alisema samaki ni zao endelevu lazima wajue kwamba wanahitaji kuzaliana, wanahitaji kukua ili waweze kuwavua kwenye saizi ambayo itawapatia wao kipato cha kutosha  hivyo ni muhimu kutunza mazingira.


Sambamba na hilo  Mkuu huyo wa mkoa Kigoma  amewataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama  ili   kuimarisha usalama katika ziwa Tanganyika kwani hali duni na tete ya usalama ndani ya ziwa inapunguza tija kwa wavuvi na wasafirishaji wa vyombo vya abiria na mizigo kwenye ziwa hilo kushindwa kufanya shughuli zao kwa tija na kuhimiza utoaji wa taarifa mapema wanapoona viashiria vya watu wanaofanya kufanya matukio ya uharamia ziwani.




Kwa upande wake Shekhe wa mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa alisema shirika hilo pamoja na kutoa misaada ya kuanzisha miradi ya kiuchumi pia limejenga misikiti 37 katika  mkoa wa Kigoma katika mpango wake wa kuimarisha dini miongoni mwa waumini wa kiislam mkoani humo.


Pamoja na hilo Shekhe huyo wa mkoa Kigomahuku akiwataka  wanufaika wa mradi huo kutumia vifaa hivyo vya uvuvi kuleta tija na kuondoa umaskini badala ya kuviuza na kugawana fedha jambo ambalo halitakuwa limefanikisha lengo lililokusudiwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI