Na Thabit Madai,Zanzibar -Matukio Daima APP
BENKI ya Watu wa Zanzibar PBZ imetenga Shilingi Bilioni 3.6 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia Wananchi katika sekta mbalimbali za Maendeleo lengo likiwa ni kurejesha faida inayopatikana kwa jamii.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kuhusu Mafanikio kwa kipindi cha Miaka Miwili, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Watu Zanzibar, (PBZ) Dkt Stella Ngoma amesema kuwa, Benki hiyo imeweka utaratibu huo lengo likiwa kuwainua Wananchi kiuchumi kutokana na faida inayopatikana ndani ya Benki hiyo.
Amesema, PBZ imekuwa na utaratibu wa kutoa Michango Mikubwa kwa Uchumi na Maendeleo ya Zanzibar pamoja na Udhamini wa matukio mbalimbali muhimu.
"Miongoni mwao ni pamoja na kudhamini ligi kuu soka Zanzibar' PBZ Premier League' kwa Mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya zaidi ya Bilion Tatu pamoja na kusaidia Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi," Amesema.
Ameongeza kuwa PBZ imefanikiwa kusaidia elimu kupitia Program ya Tokomeza Ziro Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi sambamba na kusaidia misaada mbalimbali katika Jumuiya za Watoto Mayatima na Watu wenye Mahitaji Maalum.
Hata hivyo Dkt Stella Ngoma amesema katika kuunga Mkono sera ya Serikali ya Uchumi wa Buluu PBZ imefanikiwa kusaidia jamii katika uwezeshwaji wa Wafanyabiashara ndogo ndogo pamoja na Miradi mbalimbali.
"PBZ kwa kipindi cha Miaka Miwili tumefanikiwa kuwawezesha Wafanyabiashara Wadogo wadogo na hasa katika Sekta za Uchumi wa Buluu ambapo gharama zilizotengwa na kutolewa ni Shilingi Milion 500 ikiwa ni majaribio," amefafanua Dkt Stella Ngoma.
Dkt Stella ameeleza mafanikio mbalimbali waliyapata kwa kipindi cha Miaka Miwili 2020 hadi 2022 ikiwemo kufanikiwa kuongeza rasilimali zake kwa asilimia 86 kutoka Shilingi 753 Bilion Disemba 2020 hadi kufikia Trilioni 1.4 Disemba 2022.
Amesema wamefanikiwa kuongeza kiwango cha Mikopo ya kawaida kwa Asilimia 72 kutoka Shilingi 419 Bilion Disemba 2020 hadi kufikia Shilingi 721 Bilioni kwa Mwaka 2022.
"Hata hivyo Amana za Wateja zimeongezeka kwa Asilimia 84 kutoka Shilingi 578 bilioni Disemba 2020 hadi Shilingi 1.064 Trilioni Disemba 2022," Ameeleza.
Dkt Stella amefafanua kwamba, hadi kufikia mwezi Disemba 2022 PBZ imeshika nafasi ya Sita katika utengenezaji wa faida kati ya Benki zaidi ya 44 zinazotoa huduma za kibenki Nchini Tanzania.
"Ndugu Waandishi wa Habari Benki yetu imeshika nafasi 10 katika ukubwa wa Rasilimali ni jambo la kujivunia sana lakini mafanikio haya yanapatikan kutokana na sera nzuri ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 Comments