Na Amon Mtega Mbinga.
MENEJA wa Benki ya NBC tawi la Songea Mkoani Ruvuma Frank Kilanga ameupongeza uongozi wa shule ya Sekondari ya Agustivo (High School) iliyopo Mbinga Mkoani humo kwa kuwasimamia Wanafunzi kufuata maadili mema ya desturi na tamaduni za kitanzania na kuachana na tabia za tamaduni za Nchi za magharibi.
Kilanga ametoa pongezi hizo wakati akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya wahitimu 43 wa kidato cha Sita katika shule hiyo ambao wanatarajia kuanza mitihani yao mwezi Mei mwaka huu .
Meneja huyo ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ya shule inayomilikiwa na mtu binafsi ambayo imeanzia kidato cha kwanza hadi cha Sita amesema kuwa baadhi ya shule hapa Nchini Wanafunzi wake wamekuwa wakiiga tabia za tamaduni za mataifa mengine hasa magharibi jambo ambalo linapelekea kuharibu kizazi chetu na mwisho wa siku kuwa na Vijana ambao hawana msaada kwenye jamii.
Aidha meneja huyo licha ya kuongeza kwa kusimamia maadili hayo lakini bado ameipongeza Shule hiyo kwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ambayo kwa taarifa iliyosomwa na mkuu wa Shule hiyo Mussa Mapunda kuwa hadi sasa shule hiyo imefuta sifuri na alama ya nne(division Four) ambapo malengo ni kufikia alama ya kwanza na yapili.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Mussa Mapunda akizungumzia kuhusu suala la maadili kwa Wanafunzi hao amesema kuwa uongozi wa shule hiyo umekuwa ukitumia siku za Jumapili kutoa Elimu juu ya kusimamia maadili ya Taifa letu na kuacha kuiga tabia za mataifa mengine jambo ambalo huwafanya Wanafunzi hao kuwa na maadili mema na hatimaye kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Naye mmoja wa wahitimu wa Shule hiyo David Mbunda wakati akisoma risala amesema kuwa wamelelewa vema katika shule hiyo kutokana na Miundombinu yake kuwa bora huku akisema pindi watakapokuwa wakiendelea na masomo kwenye vyuo mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu watasimamia maadili waliyofundishwa hapo shuleni ili kuwa mfano bora kwenye jamii.
Mkurugenzi wa Shule hiyo Joseph Mdaka wakati akiwashukuru Wazazi ,Walimu pamoja na mgeni rasmi ametoa zawadi kwa Walimu na wafanyakazi wengine wa Shule hiyo ambapo baadhi ya Walimu hao wamepokea fedha sh.500,000 kwa kila mwalimu ambaye somo lake amefanya vizuri na Walimu wengine walipata sh.300,000 kulingana na ufaulishaji wao huku akisema ameamua kuwapatia zawadi hizo ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao wa kuwafundisha Wanafunzi hao.
0 Comments