Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amezitaka halmashauri zote za mkoa Kigoma kuzingatia usawa wa jinsia wanapopanga na kutekeleza mipango yao ya maendeleo.
Andengenye alisema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kimkoa ilifanyika kwenye kijiji cha Kidahwe halmashauri ya wilaya Kigoma na kusema kuwa maazimio ya Beijing China ya mwaka 1995 yanapaswa kuwa dira katika kushughulikia mipango yote inayohusisha wanawake.
Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kutekeleza masuala ya kimaendeleo kwa kuzingatia usawa wa jinsia ambapo Katiba ya nchi, ilani ya uchaguzi ya CCM,sera mbalimbali kwenye wizara, dira ya maendeleo ya Taifa na mipango yote ya serikali imezingatia jambo hilo.
Kutokana na hilo alisema kuwa ofisi yake haitaki kuona Halmashauri za mkoa huo zinabagua wanawake katika kupanga na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ya mkoa huo na kwamba binafsi atakuwa anafanya tathmini kuona utekelezaji huo.
Akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake mkoa Kigoma (UWT),Agripina Buyogera alisema kuwa tangu kufanyika kwa mkutano wa Beijing kumekuwa na maendeleo kufuatia mikakati mbalimbali iliyowekwa na kina mama katika kupiga vita ukandamizaji wa wanawake uliokuwa ukifanyika.
Hata hivyo alisema kuwa bado juhudi kubwa inahitajika kuhakikisha ukombozi na maendeleo ya wanawake yanapiganiwa zaidi kwani bado yapo maeneo ambayo kuna changamoto ambazo zinafanya mpango wa kufikia asilimia 50 kwa 50 ya usawa wa jinsia unafikiwa.
Awali Katibu Tawala wa mkoa Kigoma, Albert Msovela akitoa taarifa ya mkoa wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo alisema kuwa ofisi yake imesimama usawa wa kijisnia katika utekelezaji wa mipango mbalimbali inayosimamiwa katika mamlaka za serikali za mitaa.
Msovela alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kiasi cha shilingi milioni 957.4 zimetolewa kwa makundi 114 maalum kwenye halmashauri za mkoa huo na kati yake vikundi vya wanawake 38 vilifanikiwa kupata mikopo hiyo.








0 Comments