Header Ads Widget

MRADI WA MAJI WA BILIONI 2.03 WASAINIWA MAKETE NJOMBE

 


Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE


Jumla ya wakazi 15474 wanatarajia kupata maji safi na salama katika kata za Isapulano na Iwawa Wilayani Makete Mkoani Njombe baada ya serikali kuingia mkataba wa usambazaji mabomba ya kusambaza maji ili kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 98 hadi 100.


Kaimu mkurugenzi wa mamlaka ya maji Makete mjini MAKEWASA Alphonce Kahimba amesema   kuwa mradi huo utahudumia vijiji vitano vya Isapulano,Ndulamo,Luvulunge,Iwawa na Maleutsi ambapo kwa sasa huduma ya maji inapatikana kwa asilimia 83 katika mji wa makete na saa za huduma ni chache kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya uhakika.



Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya mamlaka ya maji Njombe mjini NJUWASA Fidelis Lumato  amewataka wakazi wa kata ya Isapulano ambako ndiko kuna chanzo cha maji hayo kuendelea kutunza vyanzo hivyo ili kuwafikishia wananchi wote maji kwa uhakika.


Hata hivyo mkurugenzi wa mamlaka ya maji Njombe mjini Njuwasa ambao ni wasimamizi wa mamlaka ya maji makete mjini Mhandisi John Mtyauli amesema mradi huo wa shilingi bilioni 2.03 utakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji katika vijiji hivyo  na kuondoa adha ya mgao wa maji.


Kwa upande wake mgeni wa heshima katika zoezi hilo Juma Sweda mkuu wa wilaya ya makete amewataka wananchi hao kuanza kufikiria kuboresha maisha yao kwa kuingiza maji ndani ya nyumba zao huku akimgomea mkandarasi  sababu yoyote itakayokwamisha utekelezaji wa mradi huo.



Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo,Meneja masoko wa kampuni ya Pipes Industry Limited Hussein Chuma inayosambaza mabomba hayo amewatoa hofu wananchi hao kwani watatekeleza mradi huo haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa mkataba kwa kuwa  tayari utekelezaji unaendelea.


Wakazi wa Kata za Isapulano na Iwawa Wilayani Makete akiwemo Evelina Mahenge,Coretha Mbilinyi na Sipati Sinene wameonesha furaha yao baada ya kusaini kwa mkataba wa kusambaza maji katika maeneo yao na kwamba sasa maisha yataimarika zaidi.



Mradi huo ukikamilika unatajwa kwenda kumtua mama Ndoo kama ambavyo serikali ilisema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI