NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Profesa Patrick Ndakidemi amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani Serikali imeshatoa Bilioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali katika kata ya Mabogini.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja Ubungo Shabaha ambapo Mbunge na Diwani wa kata hiyo Bibiana Massawe waliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka miwili.
Alisema kuwa, kwa kipindi hicho kifupi, Serikali imetekeleza miradi mbali mbali katika sekta ya afya, elimu, barabara, maji na maendeleo ya jamii yenye thamani ya shilingi bilion 2.7.
Katika miradi hiyo, mradi wa kielelezo ni ule wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ambao mpaka sasa Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni moja, na kazi inaendelea.
"Mabogini mmepokea kiasi cha shilingi milioni 50 toka Serikalini kwa ajili ya ujenzi unaoendelea wa Zahanati ya vijiji vya Mji Mpya na Mvuleni kwenye sekta ya maji, tayari Serikali imeshawekeza kiasi cha shilingi milioni 500 kwa mradi wa maji katika Kata ya Mabogini" alisema Profesa Ndakidemi.
Mbunge huyo alidai kuwa ripoti yao imeonyesha kwamba vikundi vilivyonufaika na mikopo ya Halmashauri ni vingi na wanaendelea kuomba.
Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumuunge mkono Rais, Mbunge na Diwani kwenye harakati zote za kuwaletea maendeleo.
Wananchi waliohudhuria katika mkutano wa hadhara walieleza kero zao ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara, umeme, ukosefu wa maji na kutokuwepo kituo cha polisi katika eneo la Shabaha.
Akijibu kero hizo, Mbunge aliwaeleza wananchi kuwa wameiomba Serikali ijenge barabara ya Gatefonga - Mabogini - Kahe kwa kiwango cha lami huku barabara nyingine za kata zitatengenezwa na TARURA kwa kadri fedha zitakavyopatikana kutoka serikalini.
Aidha Mbunge huyo alipita kanisa katoliki Mabogini kumsalimia Paroko ambapo walimkuta akiwa na wanafunzi wa shule ya sekondari Mpirani kwenye kipindi cha dini na kupata fursa ya kuzungumza nao kwa ufupi.
Wanafunzi hao walimweleza Mbunge baadhi ya kero zinazowakabili ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mabweni kwani hivi sasa wanatembea umbali mrefu kufika shuleni.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi likiwemo somo la hisabati ambapo hivi sasa wana mwalimu mmoja tu.
Kutokana na changamoto ya mwalimu wa hesabu, Paroko wa Kanisa Katoliki Mabogini Padri Patrick Soka amejitolea kusaidia kufundisha somo la Hisabati.
Mbunge aliwaeleza wanafunzi hao kuwa amechukua changamoto yao ya uhaba wa waalimu huku alidai kuwa anataarifa kuwa shule ina mpango wa kuanzisha bweni la wasichana, na wavulana ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa bweni.
Wataalamu walioandamana na Mbunge kutoka MUWASA na idara ya maendeleo ya jamii waliahidi kusaidia wananchi kutatua kero zilizolalamikiwa.
Mwisho...
0 Comments