KITUO cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) kimewataka wananchi kuripoti vitendo vya ukatili wa ambavyo vinafanywa na baadhi ya wanajamii kwa wanawake na watoto.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu kituo hicho Dismas Chihwalo wakati akitoa elimu ya ukatili w kijinsia kwa viongozi wa Kata ya Misugusugu Wilayani Kibaha.
Chihwalo alisema kuwa vitendo hivyo vinashindwa kukomeshwa kutokana na baadhi ya wananchi kutoripoti matukio hayo yanapotokea ndani ya jamii.
"Tatizo kubwa ni watu kutotoa taarifa yanapotokea matukio haya kwani baadhi yamekuwa yakihusisha ndugu hivyo kuhofia kuwa endapo watawabainisha na hatua kuchukuliwa kutagombanisha undugu wao hali ambayo inafanya matukio hayo kuishia majumbani,"alisema Chihwalo.
Alisema kuwa pia ni jamii kufumbia macho vitendo hivyo kuhofia kuchukiwa endapo mwanajamii atajulikana kuwa ndiye aliyeripoti na mhusika kuchukuliwa hatua.
"Jamii inapaswa kutofumbia macho vitendo vya ukatili ambapo wahanga wakuu ni wanawake na watoto kwani madhara kwa wanaofanyiwa ni makubwa hasa kisaikolojia hivyo lazima watoe taarifa sehemu husika,"alisema Chihwalo.
Aidha alisema kuwa kutotolewa taarifa hizo ndiko kunasababisha athari kwa vitendo hivyo kuendelea na kusababisha hata matukio makubwa ya kikatili ikiwa ni pamoja na mauaji.
Naye Diwani wa Kata ya Misugusugu Upendo Ngonyani alisema kuwa jamii inapaswa kupaza sauti kwa kutoa taarifa juu ya vitendo hivyo ili viweze kupungua kwa wahusika kuchukuliwa hatua.
Ngonyani alisema kuwa wasihofie kwani wanaweza kutoa taarifa hizo kwa siri sehemu husika bila ya kufahamika kwani watakuwa wamesaidia kukamatwa wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wapelekwe sehemu za sheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vitendo Salehe Libebile alisema kuwa moja ya sehemu ambako kunatokea mmomonyoko wa maadili ni kamari na baa ambazo zinakesha.
Libebile alisema kuwa baa zinazokesha imekuwa ni sehemu ya vitendo visivyo na maadili vinafanyika kwani wanawake wamekuwa wakiuza miili yao na uvutaji wa bhangi.
0 Comments