Header Ads Widget

LAAC : KUNA UDHAIFU MKUBWA KATIKA MFUMO WA UKOPESHAJI NA UFUATILIAJI MAREJESHO YA MIKOPO YA 10%

 


 


NA HADIJA OMARY_ LINDI……



KAMATI ya kudumu ya  Bunge inayoshughulikia hesabu serikali za Mitaa LAAC Imeitaka ofisi ya Rais TAMISEMI  kwa kushirikiana na serikali za mikoa Nchini kutathimini upya utaratibu wa kisheria na muundo wa kitaasisi utakaowezesha usimamizi na uendeshaji bora wa mfuko wa mikopo kwa vikundi vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu  ili uweze kuleta tija iliyokusudiwa.

 

Akizungumza kwa niaba ya kamati mwenyekiti wa kamati hiyo Halima Mdee (MB) katika kuhitimisha zihara ya ukaguzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo waliyoifanya kwenye Halmashauri za Nachingwea, Mtama, na Lindi Manispaa  Mkoani   Lindi.

 

Mdee alisema licha ya mheshimiwa Rais kusisitiza fedha hizo zinazotokana na mfuko wa mikopo kwa vikundi vya akinamama , vijana na watu wenye ulemavu  kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zikopeshwe kwa tija lakini  hali ni tofauti kwa watendaji wa serikali za mitaa kwani fedha hizo zinatolewa kama zawadi kwa wakopeshwaji.

 


Alisema kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wa ukopeshaji na ufuatiliaji wa marejesho wa mikopo hiyo  hivyo serikali isipochukua hatua mfuko huu hautasaidia chochote katika kupunguza wigo wa ukosefu wa ajira Nchini kwani fedha hizo zinatumika kwa maslahi binafsi.

 

“katika hili kamati ya Bunge hesabu za Serikali za mitaa  LAAC inashauri masharti ya sheria na kanuni za usimamizi na uendeshaji wa mfuko viangaliwe upya ili kuleta tija kama lengo la serikali”

 

 

Aidha kamati inashauri kwamba miongoni mwa vigezo vya kupima ustadi wa wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kiongezwe kigezo cha ufanisi wa Mkurugenzi katika kutoa mikopo ya mfuko huo na kufuatilia ipasavyo marejesho kutokana na mikopo hiyo.

 

Alitolea mfano kwa mwaka 2021/2022 kati ya 183 zilizopo Nchi mzima  halmashauri 185 zimeshindwa kufanya marejesho ya shilingi milioni 47.5 huku taarifa walizonazo kamati hiyo kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI kwenye bajeti ya  mwaka wa fedha 2022/2023  makusanyo kwa halamashauri hizo yanatarajiwa kuwa tilioni 1.03.


“kwa hivyo asilimia 10 ya tilioni 1.03 itakuwa bilioni 100 hivyo kwa mwaka huu wa fedha bilioni 100 zinatarajiwa Kwenda kwenye vikundi vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu”


“maoteo ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri zetu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yanatarajiwa kuwa tilioni 1.300 hivyo endapo kama Serikali haitaandaa mfumo thabiti wa kusimamia na kuhakikisha fedha za walipa kodi zinazotolewa zinaenda kwa watu sahihi na kurejeshwa kwa watu sahihi hakutakuwa na maana ya mfuko huu kuwepo” alisema Mdee

 

 

Alisema hali hiyo imedhihilika wazi hata katika Halmashauri tatu za Mkoa huo wa Lindi ambazo kamati hiyo ilitembelea ambapo kwa Halmashauri ya Nachingwea  ilipaswa kuchangia kiasi cha Tsh. 254.6 mil lakini ilichangia kiasi cha Tsh, 216.03 mil. Mpaka sasa Kamati haijathibitishiwa kiasi cha Tsh. 38.6 mil sawa 15% kimeenda wapi? Ukubwa wa tatizo hili unaweza kuonekana zaidi endapo Serikali itaamua kufuatilia kiasi cha mikopo inayotolewa na kurejeshwa kila mwaka. 


 

Kikundi cha Akina Mama Kinachojulikana kwa jina la Mshikamano kilichopo Mtaa wa Naipanga kilikopeshwa mkopo kiasi cha Tsh. 18 mil lakini mpaka sasa kimeweza kurejesha Tsh. 550, 000/= ikiwa ni marejesho ya kipindi cha zaidi ya miezi 15.

 

Mdee alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama ina udhaifu katika suala hili pia. Tangu mwaka 2016/17 hadi 2020/21, Halmashauri ilitoa mikopo kiasi cha Tsh.  271.1 mil na kufanikiwa kurejesha Tsh. 121.7 mil huku Tsh. 149.3 mil zikiwa bado mikononi mwa wakopaji.


 

“Kwa mwaka 2020/21 peke yake, Halmashauri ilitoa mikopo kiasi cha Tsh. 127.1 mil na kurejesha Tsh. 88.4 mil huku kiasi cha Tsh. 38.6 mil kikiwa bado mikononi mwa wakopaji. Zaidi ni kwamba, utoaji wa mikopo hii hauzingatii uwiano wa asilimia 40:40:20 kwa vikundi vya Akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu mtawalia. Kwa mfano, katika mwaka 2020/21, mikopo ilitolewa kwa uwiano wa asilimia 60:40:0.” aliongeza

 

Kwa Manispaa ya Lindi pia  kuna udhaifu katika kusimamia na kuendesha Mfuko wa Mikopo kwa Vikundi vya Akina Mama, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Manispaa ya Lindi. Tangu mwaka 2015/16- 2020/21 pametolewa mikopo ya jumla ya Tsh228.7 mil. Lakini jumla ya kiasi kilichorejeshwa kwa kipindi hicho ni Tsh. 99.5 mil tu.

 


Utoaji wa mikopo kwa Vikundi vya Akina Mama, Vijana na Watu wenye Ulemavu kwa utaratibu uliotumika na Manispaa hiyo  kwenye Kikundi cha Akina Mama Lishe wa Soko la Sabasaba hauwezi kumkwamua mnyonge kutoka kwenye lindi la umaskini. 

 

“ Kikundi hicho kilifadhiliwa miundombinu kwa ajili ya biashara ya chakula lakini hakikupewa mtaji wa kufanyia biashara ndiyo maana kina suasua katika marejesho. Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na  Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi mnapaswa kutathmini upya namna ya kuvisaidia vikundi hivi ili vinufaike kibiashara na virejeshe mikopo vizuri.”


 

Akizungumzia mipango ya serikali juu ya mfuko huo wa mikopo kwa vikundi vya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu  Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI Deogratius Ndenjembi Alisema serikali tayari imeliona jambo hilo ambapo Katika kulifanyia kazi  Waziri  Ofisi ya Rais TAMISEMI tayari ameshaunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia mfomo mzima wa mfuko huo mikopo ya asilimia 10 ambapo utakapokuwa tayari wizara itawashirikisha wadau kwa ajili ya kuchangia maoni yao.

 

Hata hivyo Ndenjembi alisema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI tayari imeunda mfumo ambao vikundi hivyo  vitasajiliwa ndani ya mfumo ambapo itaanza kutoa mikopo na kuifuatilia kwa wale wahitaji watajisajili kwenye mfumo huo.

 

Pia mpango mwingine uliopo ni kuangalia kwa ndani  mchakato uliopo wa Sheria yenyewe kuweza kuibadili na kuweka  uwangalizi na usimamizi mzuri wa sheria yenyewe ya asilimia 10. 

 

" ni kweli katika miaka ya hivi karibuni fedha nyingi zimetoka lakini katika urejeshwaji wake  umekuwa na changamoto lakini sasa tunaangalia vile vile ukiacha  na mazingira ya sasa asilimia 4 kwa akina mama,  4 kwa vijana na 2 kwa walemavu kama inajitosheleza labda tuangalie mfumo mwingine wa kushirikishana na taasisi za kifedha ambazo  zinaweza kusimamia na kadharika" alisema Ndenjembi 

 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI