Na Amon Mtega _Mbinga.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Mdaka amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo Aziza Mangosongo kuwasimamia watu wa Tarura na Tanesco kuhakisha wanapunguza baadhi ya changamoto zinazowakabili Wananchi katika masuala ya barabara na umeme.
Agizo hilo amelitoa wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye mkutano wa Halmashauri kuu ya Wilaya ambapo taarifa hiyo imewasilishwa na mkuu wa Wilaya hiyo .
Mdaka akipokea taarifa ya utekelezaji wa ilani hiyo ambayo yenye kurasa 303 kwenye mkutano huo uliohudhuliwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda na Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini Benaya Kapinga , amesema kuwa licha ya taarifa ya utekelezaji kuwa nzuri na Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi mazuri bado changamoto ipo katika eneo la usambazaji wa umeme wa Rea Vijijini pamoja na baadhi ya barabara za Vijijini kupitika kwa shida.
Mwenyekiti amefafanua kuwa Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejitahidi katika sekta mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa Miundombinu ya Elimu hivyo ni vema katika sekta ya Umeme na Tarura zikaongeza kasi ya utendaji kazi ili kuendana na utekelezaji wa ilani.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amepongeza mkuu wa Wilaya hiyo Aziza Mangosongo pamoja na wakurugenzi wake wa Halmashauri ya Mbinga Mji na Halmashauri ya Mbinga Vijijini kwa kusimamia utekelezaji wa ilani jambo ambalo huwafanya Wananchi kuendelea kukipenda Chama cha Mapinduzi kwa kukipatia dhamana ya kushika dola.
Akisoma taarifa ya utekelezaji kwenye mkutano huo Mkuu wa Wilaya hiyo Aziza Mangosongo amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza maagizo ya chama kwa kuyafanyia kazi na kuwa katika utekelezaji wa ilani maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi na kuwa amepokea maagizo ya chama kuhusu suala la Tarura na Tanesco.
Kwa upande wake katibu wa CCM Wilaya ya Mbinga Mary Mwenisongole amewataka madiwani wa Wilaya hiyo kwenda kufanya mikutano na Wananchi kwenye kata zao ili kuwaelezea jinsi utekelezaji wa ilani ulivyofanyika.
Katibu Mwenisongole amesema kuwa kumekuwepo kwa baadhi ya madiwani wanapokea taarifa ya utekelezaji lakini kwenye kata zao hawapeleki ujumbe wa utekelezaji huo jambo ambalo huwafanya baadhi ya Wananchi kuibua hoja zisizokuwa za msingi.
0 Comments