Na Fadhili Abdalla,Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimetoa maelekezo kwa kamati za siasa na halmashauri kuu za kata na wilaya kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafukuza uanachama wenyeviti wa serikali za vijiji na halmashauri zao za vijiji kwa matumizi mabaya ya madaraka ambayo yamesababisha migogoro mikubwa ya ardhi na hali tete ya usalama kwenye maeneo yao.
Maelekezo na maagizyo hayo yametolewa na Katibu wa CCM mkoa Kigoma,Mobutu Malima wilayani Buhiwe mkoani Kigoma katika kikao na wenyeviti wa vijiji,madiwani, makatibu na wenyeviti wa kata wa CCM akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na viongozi wa chama na serikali wilayani humo.
Malima ambaye aliongoza na wajumbe wa sekretariet ya CCM ya mkoa Kigoma alisema kuwa matumizi mabaya ya mihuri na nafasi zao kama wasimamizi wa maendeleo na wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama ya vijiji wamefanya mambo makubwa ambayo hayapo kwenye mamlaka na madaraka yao.
Katibu huyo wa CCM mkoa Kigoma alisema kuwa moja ya jambo kubwa na baya kabisa ni uuzwaji wa maeneo bila kufuata sheria wala tarattibu zilizowekwa na enyeviti hao wamekuwa wakifanya mambo hayo bila kushirikisha halmashauri zao za vijiji.
Alisema kuwa wenyeviti hao wamekuwa wakiuza maeneo bila kufuata vikao ikiwemo kuuza zaidi ya uwezo wa kisheria unaowaruhusu kufanya hivyo, kuingia wafugaji kinyemela sambamba na kukaribisha raia wa nje bila kufuata taratibu za nchi huku vitendo vya rushwa ikielezwa kuwa ndiyo maisha yao.
“Tabia hii ya wenyeviti wa vijiji ni tatizo kubwa na hao ndiyo wanaokipaka matope chama kwa mambo ya hovyo wanayofanya, natoa agizo kwa kamati za siasa za kata kuwaangalia viongozi na kutowarudisha tena kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 maana hao ni mzigo kwa chama,”Alisema Katibu huyo wa CCM mkoa Kigoma.
Awali Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Buhigwe,Erneo Dyagula akizungumza kwenye mkutano huo na viongozi wa kata na vijiji alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na viongozi wa vijiji ikiwemo kugombea mipaka ya vijiji na vitongoji na uuzwaji holela wa maeneo imeleta changamoto kubwa kwenye suala la maendeleo kwa kuwafanya wananchi wengi kugoma kujitolea kwenye shughuli za miradi.
Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Buhigwe alisema kuwa viongozi wa vijiji kushindwa kuitisha mikutano mikuu ya vijiji kwa ajili ya kusoma mapato na matumizi na kueleza maendeleo ya shughuli za maendeleo kwenye vijiji imeondoa imani ya wananchi kwa viongozi hao na kuonekana kuwa ni viongozi wasiofaa mambo yanayozua migogoro kila siku.
Alisema kuwa ni lazima viongozi wa chama na serikali na mamlaka zao za nidhamu zichukue hatua kukabiliana na hali hiyo lakini pia ni lazima halmashauri isimamie masuala ya utumishi na utawala bora kwa kueleza wajibu, majukumu na mipaka ya viongozi wa vijiji ili kuepusha vurugu kubwa na matumizi ya madaraka ambayo hayapo kwenye nafasi ya viongozi hao.
Akizungumza kwenye Mkutano huo Kaimu Mkuu wa wilaya Buhigwe, Kanali Isack Mwakisu alisema kuwa wajibu wa kushughulikia migogoro ya mipaka ya vijiji na vitongoji ni mkurugenzi wa Halmashauri na wataalam wake na kwamba wenyeviti wa vijiji hawana nafasi katika kuamua migogoro hiyo kisheria.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa Mkurugenzi na wataalam wake wanayo nafasi kubwa ya kukaa na kuwapa maelekezo wenyeviti hao wa vijiji lakini kuchukua hatua mapema kunapotokea utendaji unaokwenda kinyume cha sheria ikiwemo uuzwaji wa maeneo usiozingatia sheria.
Akieleza kuhusiana na maelekezo ya Katibu wa CCM mkoa kwa wenyeviti wa vijiji Mwenyeviti wa CCM kata ya Mgera wilaya ya Buhigwe,Ally Maliti alisema kuwa baadhi ya viongozi wamejawa na ubinafsi hali inayowafanya kutotaka kufuata taratibu za mamlaka na madaraka ya nafasi zao wengine wakitumia ubabe katika kuongoza.
Alisema kuwa hata hivyo wengi wao hawana semina na miiko ya uongozi ndiyo maana migogoro mingi inatokea na viongozi wanashindwa kusimamia vizuri utatuzi wa migogoro hiyo kwa maslahi ya watu wote.
0 Comments