Na Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP_MOSHI
Vijana katika wilaya ya Moshi Vijijini wamesema kuongezwa kwa fedha za kujikimu kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu kutaenda kuwapunguzia changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa zikiwakabili hapo awali na hivyo kuwaweka katika hali ya utulivu katika masomo yao.
Pia hata hatua ya kufikiria kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma elimu ngazi ya cheti na astashahada nayo inaelezwa ni njia mojawapo katika kukuza wigo wa kuwapata wasomi na wataalam mbali mbali ambao watashiriki kuikuza nchi katika nyanja mbalimbali.
February 11.2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia ombi la viongozi wa shirikisho la wanafunzi wa Ttaasisi za elimu ya juu Tanzania (Tahliso) la kutaka kuongezewa fedha za kujikimu kutoka Sh8,500 kwa siku hadi Sh10,000.
Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM)wilaya ya Moshi Vijijini Yuvenail Shirima amesema hatua iliyofikiwa na rais Samia ni mwanga mpya katika kuzalisha wasomi hapa nchini.
"Sisi kama vijana tuseme tumepokea kwa mikono miwili kauli ya rais Dkt Samia ya kuongeza kiwango hicho cha pesa'boom'kutoka 8500 hadi 10000 hapa ni kuwa vijana waliopo vyuoni wanaenda kupunguziwa ukali wa maisha"amesema
Shirima anasema kuwa hata wanafunzi wanaosoma ngazi za cheti na astashahada nayo wameanza kufikiriwa namna ya kupata mkopo hivyo kunaenda kujenga wigo mpana zaidi katika kuzalisha wasomi.
"Tumeona ambavyo rais ana nia nzuri kwa vijana ambapo hata wanaosoma diploma au cheti nao hapo mbeleni wataenda kupatiwa mikopo hii ni ishara kuwa vijana wengi wataenda kujiunga na masomo ya juu bila vikwazo tena"amesema
Kwa mujibu wa Shirima ni kuwa umoja huo ndio walezi wa seneti ya vyuo na vyuo vikuu ambapo walipokea mapendekezo na kuweza kuyafikisha sehemu husika ambapo kwa sasa yamepatiwa suluhisho.
"Sisi umoja wa vijana ndio walezi wa seneti ya vyuo na vyuo vikuu haya tumekuwa tukiyazungumza uzuri yamefanyiwa kazi na hapa hata kama changamoto Kwa waliopo vyuoni hazitaisha ila zitaenda kupunguza kwa kiwango fulani"anasema Shirima
Februari 11, 2023 Ikulu jijini Dodoma, Rais Samia alikutana na viongozi wa Tahliso na Zahlife kwa upande wa Zanzibar ambapo aliwapa nafasi ya kuuliza maswali na kuzungumza nao kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu.
Katika mkutano huo, Rais wa Tahliso, Frank Nkinda amewasilisha maombi yao kwa Rais Samia ili aweze kuwasaidia wanafunzi hapa nchini kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.
Moja ya maombi yaliyowasilishwa na Nkinda ni pamoja na kuongezewa kiasi cha fedha za kujikimu kinachotolewa na serikali kwa wanafunzi kwa siku kutoka Sh8,500 za sasa hadi kufikia Sh10,000 kwa sababu maisha yamepanda.
0 Comments