Teddy Kilanga _Arusha
Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Jenista Mhagama ameonya baadhi ya watumishi wasio na maadili haswa maeneo ya mipakani kuharibu mifumo ya Tehama na kudai mtandao upo chini huku wakisababishia serikali hasara badala yake wanapitisha vitu kimya kimya .
Akizungumza jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya kikao kazi cha tatu cha Mamlaka ya Serikali Mtandao ambapo Kauli mbiu "Mifumo Jumuishi ya Tehama kwa utoaji Bora wa Huduma za Umma" kilichojumisha washiriki zaidi ya 1600 kutoka idara mbalimbali za serikali.
Waziri huyo alisema baadhi ya wakuu wa vitengo hawana weledi katika kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma na kutolea mfano maeneo ya mipakani wataalamu kudai mtandao upo chini wakati kunavitu vinapita kimya kimya.
"Kwanini mitandao ya simu ipatikane lakini ukifika mipakani unaambiwa mtandao upo chini haswa Tehama, kunashida ya watumishi kutokuwa na uzalendo hivyo acheni kupiga dili saidieni serikali kupata mapato acheni kucheza na mkongo wa Taifa au kung'oa baadhi ya vitu kwakisingizio cha mifumo sasa tunawashughulikia wanaofanya michezo hii,"alisema Waziri Muhagama.
Muhagama alisema kuwa endapo Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ikijipanga vema inauwezo wa kusogeza huduma za Tehama hadi ngazi za vijiji ili kuwezesha wananchi kupata maendeleo mbalimbali.
"Endapo eGA ikisogeza huduma hizo kwa wananchi serikali itaweza kupata taarifa mbalimbali na kusimamia sera kwa ujumla na viwango vya ubora vinavyotakiwa,"alisema Waziri Muhagama.
Aidha alisisitiza watumishi kusimamia na kuzingatia kanuni na miongozo ili kuzingatia usalama wa matumizi ya Tehama na kutoa maagizo kwa taasisi zote zisizojiunga na mfumo wa eGA kujiunga mara moja ili kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Alisema mara baada ya kikao hicho lazima taasisi na mashirika kuomba na kupewa kibali na eGA kabla ya kuanza kutekeleza mifumo yao ikiwemo kuwa na vikao vya kitaasisi kila mwaka kwaajili ya kufanya tathimini ya utendaji kazi unaohusu serikali mtandao ikiwemo wakuu wa idara na vitengo kukutana na watumishi ili kubaini changamoto za Tehama.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndombi alisema mafunzo hayo yatawasaidia wakurugenzi,wakuu wa taasisi, Makatibu Tawala na watumishi wengine kutumia serikali mtandao ili kuwezesha serikali kupata mapato mengi ikiwemo kuondokana na matumizi ya makaratasi badala yake wawe kidigitali zaidi.
0 Comments