Na Amon Mtega,Mbinga.
SHULE ya Sekondari Mahenge Amcos inatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya jengo la utawala kukamilika pamoja na madarasa manne huku madarasa sita yakiwa hatua za mwisho na maabara.
Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo mwenyekiti wa Chama cha msingi Mahenge Amcos kilichopo Kijiji cha Mahenge kata Litembo tarafa ya Mbuji Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Julius Mbunda amesema kuwa shule imeshafikia vigezo kwa kuanza kupokea wanafunzi kinachosubiriwa ni vibali kutoka Serikalini.
Mwenyekiti Mbunda amesema kuwa pindi vibali vikikamilika shule hiyo itaanza mara moja kuwachukuwa wanafunzi kwa kuwa vitu muhimu vimekamilika ikiwemo jengo la utawala.
Mbunda amefafanua kuwa Sekondari hiyo ni mali ya Chama cha msingi Mahenge Amcos imejengwa kwa fedha za wahisani wa Ujerumani ambao wamekuwa wateja kwenye Amcos ya Mahenge kwa kununua kahawa ya wanachama hao ikiwa kama sehemu ya bonasi yao.
Amesema kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi huo wanachama wote walikubaliana kuwa fedha inayotolewa na wahisani hao itumike kwa kujengea shule ikiwa ni sehemu ya kuungamkono jitihada za Serikali katika suala zima la Elimu.
Mwenyekiti huyo akielezea muundo wa shule hiyo amesema kuwa itaanza kuwa ya kutwa kwa kuchukua wanafunzi wa jinsia zote wa kiume na wakike na kuwa siku za mbele wataona namna ya kujenga mabweni kwa kuwa kumekuwepo na eneo kubwa la ujenzi.
Aidha ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa pindi itakapoanza shule hiyo basi wasisite kupeleka watoto wao kwa kuwa shule hiyo imejengwa Kijiji cha Mtama kata ya Utili katika Halmashauri ya Mbinga mji.
0 Comments