Header Ads Widget

RC BABU "WALIOVAMIA UWANJA WA NDEGE MOSHI NA KUJENGA MAKAZI WAONDOKE"



NA WILLIUM PAUL, MOSHI


WANANCHI wote waliovamia katika eneo la uwanja wa ndege wa Moshi mkoani Kilimanjaro na kujenga makazi wametakiwa kuondoka katika maeneo hayo na kupisha ukarabati wa ujenzi wa kiwanja hicho unaoendelea kwa sasa.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alipotembea kiwanja hicho kujionea shughuli za ukarabati zinazoendelea akiambatana na wajumbe wa bodi ya barabara mkoa wa Kilimanjaro.



Babu alisema kuwa, Serikali imetoa zaidi ya Bilioni 12 kwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hicho ambapo kukamilika kweka utachangia kuongeza kipato cha mkoa na Taifa.


"Tumesikia hapa uwanja huu unatakiwa kuwekewa fensi lakini changamoto ni baadhi ya wananchi ambao wamevamia katika eneo la uwanja na kujenga makazi sasa nakuagiza Mkurugenzi wa manispaa hakikisha watu hao wanaondoka mara moja ili kupisha shughuli za ukarabati zinazoendelea katika kiwanja hiki" alisema Babu.



Mkuu wa mkoa alisema kuwa, uwanja huo wa ndege ni wa muda mrefu lakini ni sehemu muhimu kwa mkoa hivyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu kuona umuhimu wa kuufanyia ukarabati uwanja huo.


Babu alimtaka Mkurugenzi kuhakikisha wale wote waliovamia uwanja huo wanaondoka ili kabla ya Mkandarasi kukabidhi uwanja huo Novemba mwaka huu awe ameshaweka uzio kuzunguka uwanja huo.



Alisema kuwa, kukamilika kwa ukarabati huo utapelekea watalii wengi wanaokuja nchi kutumia uwanja huo kuwa karibu na mlima Kilimanjaro.


Babu alitumia nafasi hiyo kumpongeza mkandarasi wa ujenzi wa uwanja huo Rocktronic kwa kufanya kazi kwa uzalendo japo anapitia katika changamoto ya wananchi kuvamia eneo la uwanja.



Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa barabara nchini mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio wasimamizi wa ukarabati huo wa uwanja, Mhandisi Motta Kyando alisema kuwa, malengo ya mradi huo ni kuboresha usafiri wa anga kwa ajili ya kuinua pato la Taifa kupitia sekta ya Utalii.


Mhandisi Motta alisema kuwa, kwa kuzingatia umuhimu wa viwanja vya ndege, ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Moshi utaleta matokeo chanya ya ongezeko na kukuza sekta ya utalii.



Alisema kuwa, mkataba wa ukarabati wa kiwanja hicho ulisainiwa Septemba 30 mwaka jana na kuanza rasmi Novemba 18 mwaka jana ambapo unategemewa kukamilika Novemba 18 mwaka huu.


"Kulingana na usanifu maboresho ya kiwanja cha ndege cha Moshi yanahusisha kufanya ukarabati wa njia mbili za kutua na kurukia ndege pamoja na ujenzi wa maeneo ya usalama, maboresho ya maegesho ya ndege, ujenzi wa barabara ya kuingia na kutoka uwanjani, kuweka uzio wa usalama katika kiwanja pamoja na kutengeneza barabara ya mzunguko ndani ya kiwanja na kujenga mitaro na kalvati za kutolea maji" alisema Mhandisi Motta.

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI