Header Ads Widget

PATRICK BOISAFI "MAADHIMISHO YA KUZALIWA KWA CHAMA CHA MAPINDUZI TUNAYATUMIA KUJISAHIHISHA"



NA WILLIUM PAUL, SAME.


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema kuwa sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM zimekuwa zikitumika kwa wanachama kujikumbusha na kujisahihisha pale walipokosea ili kuendelea kushuka Dola.



Boisafi alitoa kauli hiyo jana katika sherehe za maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi yaliyofanyika katika kata ya Hedaru wilayani Same ambapo alisema kuwa, chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kufanya maadhimisho ya kuzaliwa kwa chama kila mwaka Februari 5.



Alisema kuwa, kupitia maadhimisho hayo wamekuwa wakijitafakari kama viongozi na wanachama wa CCM pale walipotoka na wanapokwenda pamoja na kujisahihisha pale walipokosea.



Mwenyekiti huyo alisema kuwa, lengo la Chama chochote cha Siasa ni kushika Dola hivyo CCM itaendelea kuwahudumia wananchi kwa kutafuta majibu ya matatizo yanayowakabili wananchi ili waendelee kukiamini chama hicho na kuendelea kushika Dola.



"Natambua yapo matatizo ambayo yanawakabili wananchi sasa niagize viongozi wa Chama kuanzia shina, matawi, kata, wilaya na mkoa kufanya mikutano na wananchi na kusikiliza kero zao na zile zilizopo katika levo yenu zipatieni majibu na zile msizoziweza mzipeleke panapohusika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi" alisema Boisafi.



Aidha Boisafi alitumia pia mkutano huo wa hadhara kuwataka wanachama wa CCM kujijengea tabia ya kusoma katiba, miongozo na kanuni za chama na Jumuiya zake ili kutambua wajibu wao ndani ya chama ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake.



Pia Mwenyekiti huyo aliwataka wanaccm na wananchi kuhakikisha miradi inayojengwa katika maeneo yao inajengwa kwa kiwango kinachostahili pamoja na thamani ya fedha iweze kuonekana.


Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kuwa, chama cha Mapinduzi ni chama madhubuti na ndicho chenyekuleta amani katika Taifa.



Babu alisema kuwa, Serikali ya chama cha Mapinduzi imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi na kuwataka wanaccm kutembea kifua mbele.



Aidha Mkuu huyo wa mkoa alitumia maadhimisho hayo kuwataka Wazazi wenye watoto wa umri wa kwenda shule kufanya hivyo kwani Serikali imeshatimiza wajibu wake wa kujenga madarasa pamoja na kuleta walimu.



"Niwatake Wazazi wenyewatoto ambao wanaumri wa kwenda shule na bado hawajawapeleka kufanya hivo maramoja kabla hawajachukuliwa sheria na nikimkuta mtoto mwenye umri wa kwenda shule anachunga mifungo nitamchukua hapohapo" alisema Babu.



Sherehe hizo za maadhimisho ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro zilienda sambamba na kupanda miti katika kituo cha Afya Hedaru, uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya chama tawi la Mbuyuni pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi ofisi ya chama kata ya Hedaru.

Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS