Na Fadhili Abdallah,Kigoma
ZAIDI ya vijana 50 kutoka manispaa ya Kigoma Ujiji wanatarajia kunufaika na mradi wa ujasiliamali wa utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na taka ngumu ikiwa ni sehemu ya mpango wa utengenezaji ajira kwa vijana.
Msimamizi wa miradi wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya AfriCraft, Kelvin Nicholous akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye na wajumbe sita wa kamati ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya Bunge la ujerumani wakati wa uzinduzi wa mradi huo mjini Kigoma.
Nicholous alisema kuwa wakati huu ambapo mradi unazinduliwa jumla ya vijana wanane wameanza kujishughulisha na shughuli mbalimbali za utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na mabaki ya matumizi ya mifuko ya sement, chupa tupu, matairi ya magari na mabaki ambayo yanaweza kutengeneza bidhaa.
tukiwasaidia kwa ushauri wa kitaalam na misada ya mitaji hivyo tuanatarajia zaidi ya vijana 50 watakuwa kwenye utekelezaji wa mpango huo,”Alisema Nicholous kutoka AfriCraft.
Mkuu wa Msafara wa kamati hiyo ya Bunge la Ujerumani, Knut Gerschau alisema kuwa serikali ya Ujerumani kupitia ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania umetoa kiasi cha shilingi milioni 23.3 katika mradi huo unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi milioni 28.8.
Gerschau alisema kuwa wamevutiwa na uanzishwaji na utekelezaji wa mradi huo ambao unagusa mambo mhimu ambayo yanagusa maisha ya kila siku ya vijana nchini ikiwemo suala la utunzaji mazingira na ajira kwa vijana hivyo anaamini kuwa itasaidia kuajiri vijana ambao hawakuwa na shughuli za kuingiza kipato.
Akizindua mradi huo Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengenye alisema kuwa serikali ya mkoa imefurahishwa na kuanza kwa mradi huo ambao unalenga mambo muhimu ya mazingira na ajira kwa vijana ambayo serikali imekuwa ikiyasimamia kwa karibu.
Andengenye alisema kuwa anaamini mradi huo utasaidia kuweka mji kwenye hali ya usafi kutokana na bidhaa zitakazokuwa zinakusanywa kutumika kwenye utengenezaji wa bidhaa hivyo uchafu huo utakuwa na maana kwa maana nyingine badala ya kutupwa na kuchangia kuufanya mji kuwa mchafu na kuharibu mazingira.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa mkoa Kigoma alisema kuwa ajira kwa vijana zitakazotokana na kuanzishwa kwa mradi huo ni muhimu na kuziomba halmashauri zote mkoani humo kuunga mkono juhudi hizo na kuwapatia vijana ambao watajifunza ukusanyaji na utengenezaji wa bidhaa hizo kuwa sehemu ya ajira hivyo kituo hicho kiwe kama kituo cha mafunzo.
0 Comments