NA HADIJA OMARY LINDI.
MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi,imemuhukumu mkazi wa Kata ya Mnolela katika halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi ,Mussa Mohamed Kamba (25) kutumikia kifungo cha miaka (30) Jela,baada ya kukutwa na na hatia ya kubaka binti wa miaka 11.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi mfawidhi mwandamizi wa Mahakama hiyo,Conslota Singano baada ya kuridhishwa pasipo na shaka ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa mashitaka.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo,mshitakiwa Mussa kamba alipewa nafasi ya kujitetea,itakayoishawishi Mahakama isimpe adhabu kali kwa kosa linalomkabiri mbele yake na kuiomba Mahakama impunguzie adhabu na kuwa hatarudia tena .
Upande wa mashitaka uliiomba Mahakama hiyo utoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine kwa kuwa unyanyasaji wa kingono unazidi kushika kasi na kuhalibu ndoto za mabinti na watoto wadogo.
Hakimu Singano akitoa hukumu katika kesi hiyo ya kosa la kubaka kinyume na vifungu vya 130 (1)(2)(e) na 131 (1) vya kanuni ya adhabu sura ya 16 rejeo la 2022
alisema amesikia maombi ya pande zote,lakini kutokana na Sheria kumfunga mikono akamuhukumu mshitakiwa kifungo cha miaka (30) Jela.
Mwanzoni ilidaiwa Mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa Serikali, Godfrey Mramba kwamba mnamo 16/10/2022 katika eneo la Mtama Mtuhumiwa alimbaka binti wa miaka 11.
Mramba alieleza Mahakamani hapo kuwa mshitakiwa wakati anatekeleza kosa hilo alitumia mbinu ya kumtuma rafiki wa mhanga akamuite na baada ya mhanga kuitwa mshitakiwa alimuingiza chumbani kwake na kisha kumuwekea nguo mdomoni na baadae kumfanyia ukatili huo.






0 Comments