Halmashuri ya Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu imelenga kutumia kiasi cha Sh5.4 Bilioni katika utekelezaji wa Miradi mbali mbali ya Maendeleo ikiwemo ujenzi wa Vyumba vya Madarasa, Nyumba za Walimu, Hospitali na Zahanati za Kata pamoja na Miundombinu ya Barabara katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa kutoa Taarifa ya Fedha na Matumizi kutoka katika Kamati ya Fedha na Utawala, Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bw. Msabi Maganiko alisema kuwa Halmashauri hiyo ilipitia mpango wa manunuzi wa mwaka 2022/2023 ambao ulikuwa na manunuzi ya Bidhaa, Huduma zisizo za Kitalaam na Ujenzi zilizokuwa na Jumla ya Sh5.2 Bilioni.
Alisema kuwa Halmashauri ilipitisha Mpango wa Manunuzi wa Mwaka 2022/2023 ambao ulikuwa ni Manunuzi ya Bidhaa, Huduma zisizo za Kitalaam na Ujenzi wa Miundombinu mbali mbali ikiwemo Barabara, Madaraja, Ujenzi wa Madarasa kwa Shule za Serikali, Hospitali za Wilaya na Zahanati za Kata ambapo mpango huo uliokuwa na jumla ya Sh5,169,736,095.
Pia, Bw. Maganiko alisema kuwa Halmashauri hiyo imepanga kufanya Ununuzi wa Vifaa vingine vitakavyo leta tija kwa Wakazi wa Halmashauri hiyo ikiwemo ununuzi wa Gari aina ya Tipper Isuzu kwa ajili ya mradi wa kufyatua Matofali ya Biashara pamoja na miradi mingine itakayo ongeza pato la Halmashauri hiyo.
“Gari hili halikuwemo katika Mpango wa manunuzi. Hivyo kuna Bajeti imetengwa ya Sh162 Milioni kwa ajili ya ununuzi wake. Hivyo nawasilisha suala hili ili liweze kujadiliwa na kujumuishwa katika Mpango wetu na kufanya mpango huo kuongezeka na kuwa na jumla ya Sh5.4 Bilioni,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. John Mlenya amesisitiza katika kuongeza juhudi kwa Watumishi Umma wa Halmashauri hiyo na Watendaji wengine katika ukusanyaji wa Mapato na kuziba mianya ya Upotevu wa mapato ili Wananchi waweze kupata Huduma muhimu za Kijamii zitokanazo na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Pia aliwataka Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kusoma Taarifa za Mapato na Matumizi katika Mikutano ya kisheria ya kila Robo Mwaka ili kuleta ufahamu na uelewa kwa Wananchi kuhusu fedha zinazotolewa na zinavyotumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
“Niwatake pia Watendaji wa Kata na Vijiji wote kufanya Kazi na kuwajibika kikamilifu hususani kwa kusoma Taarifa za Mapato na Matumizi ya Fedha zote zinazotolewa na Serikali, Wafadhili na Wahisani mbalimbali pamoja na michango na nguvu za Wananchi kwa lengo la kuongeza uwajibikaji, uwazi na kuleta imani kwa Wananchi,” alisema.
Kwa pande wake, Mbunge wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bi Lucy Sabu amewataka pia Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Vikao na Mikutano hiyo ya vijiji kwa ajili ya kujadili ajenda ya Taarifa ya Mapato na Matumizi na kuwaomba washirikiane na Kamati za Siasa za Kata na Vijiji ili kutekeleza ipasavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Kwa kufanya hivyo pia itawawezesha Wananchi kushiriki katika kuchangia na kutekeleza Miradi mbalimbali mara baada ya kujionea na kuhakikisha namna Fedha hizo zinavvotumika kutekeleza vizuri miradi husika na hatimaye kuleta maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii kwa Wananchi,” alisema.
0 Comments