Header Ads Widget

CCM KIGOMA YAICHONGEA TFS KWA WAZIRI MKUU UPORAJI MAZAO YA WANANCHI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa mkoa Kigoma akizungumza wakati wa maadhimisho ya kimkoa ya sherehe ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM.

Na Fadhili Abdallah,Matukio Daima Kigoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimelaani vitendo vinavyofanywa na askari wa Wakala wa misitu Tanzania (TSF) kupora mazao ya wakulima wakati wa mavuno kwa tuhuma za kuingia maeneo ya hifadhi na kumuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo vya TSF.


Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma,Jamal Tamim alitoa ombi hilo kwa Waziri Mkuu Majaliwa wilayani Kasulu wakati wa maadhimisho ya kimkoa ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM na kusema kuwa vitendo hivyo vya TFS vinaichonganisha serikali na wananchi.


Tamim alisema kuwa inashangaza kuona kuwa TFS wanashindwa kuchukua hatua mapema kwa wavamizi hao wanapoingia kwenye maeneo hayo ya hifadhi na kuwaacha walime hadi mazao yanapofikia kuvunwa ndipo wanaingia maeneo hayo na kutaifisha mazao ya wananchi lakini kukiwa hakuna taarifa zozote kwa mamlaka za wilaya na mkoa wala kujulikana mazao hayo yanapelekwa wapi.



“Mh.Waziri Mkuu huu ni uporaji na kinyume cha maadili kwa watendaji wa umma ni vizuri viongozi mkachukua hatua kukomesha jambo hili maana kama maeneo

yamehifadhiwa ijulikane na watu wazuiwe kuingia kwa kufuata sheria lakini TFS wasisubiri wananchi walime ndiyo waingie kwenye maeneo hayo na kuwatimua huku  wakipora mazao yao,”Alisema Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa Kigoma.


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa akitoa maelezo kuhusiana na jambo hilo amesema kuwa haikubaliki vitendo hivyo na kinyume cha taratibu za utendaji na kwamba ametaka kuacha kufanya vitendo hivyo mara moja.


Majaliwa ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya CCM na Mlezi wa mkoa Kigoma amewataka wakuu wa wilaya za mkoa Kigoma kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza madaraka yao ikiwemo kusimamia masuala ya ulinzi na usalama na kuratibu shughuli zote zinazofanywa na TFS kwenye maeneo yao.


Kiongozi amewataka askari wa TFS kutofanya operesheni zozote kwenye misitu kuwaondoa wananchi hadi suala hilo liwasilishwe kwa wakuu wa wilaya na kuratibiwa na kamati za ulinzi na usalama za wilaya ikiwezekana wakuu wa wilaya washiriki kwenye mazoezi hayo.

Pamoja na hilo alisema kuwa amechukua jambo hilo na kulipeleka kwenye mamlaka za nidhamu za watendaji hao wa TFS lakini pia akiwataka wananchi kufuata sheria na kutoingia kufanya shughuli zozote kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za misitu na vyanzo vya maji.


Jamal Tamim Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma akiongea mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  kwenye maadhimisho ya kimkoa ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM.

(Picha na Fadhili Abdllah)

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS