Header Ads Widget

UVCCM MANISPAA YA MOSHI YAWAJIA JUU WANAOTAKA KUJIMILIKISHA MALI ZA CCM.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro umewaonya wanachama wa CCM wenye dhana ya kumiliki miradi ya chama hicho kuacha mara moja kwani hawatawafumbia macho watu hao.


Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Umoja huo, Sadath Ndibalema alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema kuwa, moja ya jukumu kubwa la Umoja wa vijana wa CCM ni kulinda mali za chama na viongozi wake.



Ndibalema alisema kuwa, ipo miradi ambayo inamilikiwa na chama cha Mapinduzi lakini wapo watu wamezuka na kutaka kujibinafsisha miradi hiyo na kudai kuwa UVCCM itapambana kuhakikisha miradi hiyo inaendelea kuwa chini ya himaya ya CCM.


"Jukumu kubwa la UVCCM ni kulinda mali za chama hivyo niwaombe watu watambue mali hizi sio za mtu binafsi na tutahakikisha zinatumika vizuri kwa ajili ya maslahi ya chama na zitumike zinavyotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa" alisema Ndibalema.



Mwenyekiti huyo alisema kuwa, wapo pia baadhi ya Wanachama ambao wamejisahau na kudhani wao ni wakubwa kuliko CCM na kutoa kauli zisizofaa wakidhani CCM inaogopa ushindani na kuwataka kutambua hakuna aliyemkubwa kuliko CCM na chama kipo tayari wakati wowote kupambana.


Akizungumza swala la Rais Dkt Samia Suluhu Hasani kuruhusu mikutano ya hadhara alisema kuwa wao kama Umoja wa vijana wanaunga mkono maamuzi hayo ya kiungwana na hiyo ni hatua muhimu ya CCM katika ulezi wa vyama vingine vya siasa.



Alisema kuwa, CCM kimekuwa chama cha kilezi kwa vyama vya siasa na ndio maana walikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa na bado imeendelea kuvilea vyama hivyo.


Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM manispaa ya Moshi, Arafat Mbiruka alisema kuwa ndani ya chama manispaa ya Moshi wameendelea kufanya maboresho makubwa ya kiuchumi hasa katika miradi inayomilikiwa na chama cha Mapinduzi ili iweze kuleta tija na kutimiza ndoto ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Dkt Samia Suluhu Hasani ya kuhakikisha chama kinajitegemea.



Mbiruka alisema kuwa pia wameendelea na mipango ya kuongeza miradi na kudai kuwa UVCCM manispaa itaendelea kuhakikisha inalinda miradi hiyo pamoja na kuwalinda viongozi wake kuanzia ngazi ya wilaya mpaka mkoa.

"Tunaunga mkono na kupongeza maamuzi ya Mwenyekiti wetu kuruhusu mikutano ya hadhara sasa tunawasihi viongozi wa vyama vya siasa kufanya mikutano kistaarabu na kukosoana kwa maslahi mapana ya wananchi" alisema Mbiruka.

Aidha alisema kuwa, Umoja huo unampango wa kuanzisha vibanda vya biashara mwaka huu ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza Machi mwaka huu na kukamilika ifikapo Disemba ili kuongeza mapato ndani ya chama na Jumuiya.

Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI