Header Ads Widget

UVCCM MANISPAA YA MOSHI WATANGAZA KIAMA KWA WANAOBEZA KAZI ZINAZOFANYWA NA SERIKALI.



NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

 

VIJANA wa Chama cha Mapinduzi manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wamesema kuwa hawatakubali kuona kazi zinazofanywa na Serikali chini ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hasani zikibezwa au kukandamizwa.

 


Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa UVCCM manispaa hiyo, Sadath Ndibalema wakati wa zoezi la upandaji miti katika shule ya Msingi Mwenge ikiwa ni maadhimisho ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi.

 


Ndibalema alisema kuwa, serikali imekuwa ikifanya mambo makubwa ikiwamo kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi hivyo kila mwananchi anawajibu wa kuhakikisha anaunga mkono jitihada hizo kwa kulinda miradi hiyo.

 


“Fedha nyingi zimekuwa zikitolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali hivyo sisi kama vijana wa chama cha mapinduzi tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha tunalinda miradi hiyo pamoja na kuhakikisha inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa hivyo hatutamvumilia yeyote anayetaka kuihujumu miradi hiyo” alisema Ndibalema.

 


Alisema kuwa, kutokana na hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi kwa sasa viongozi wa juu wa Serikali wameshatoa maagizo kwa wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi kupambana na hali hiyo hivyo wao kama UVCCM katika kuadhimisha kuzaliwa kwa CCM wameamua kupanda miti ya matunda katika shule ya msingi Mwenge.

 


Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM manispaa ya Moshi, Arafati Mbiruka alisema kuwa, vijana wa chama cha mapinduzi manispaa ya Moshi wameamua kuboresha mazingira pamoja na kuboresha lishe bora kwa kupanda miti hiyo ya matunda ambapo itawasaidia wanafunzi kupata matunda pamoja na kivuli.

 


Alisema kuwa, swala la uoteshaji miti ni la lazima na sio hiari kwa kila mwananchi ili kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yameathiri kwa kiasi kikubwa ulimwengu mzima.

 


Aidha alitumia pia nafasi hiyo kuwataka wakuu wa taasisi za Serikali na Umma kuwa tayari katika kutekeleza maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Kitaifa ili kusema kauli moja.

 


Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Mwenge, Helena John alisema kuwa, kitendo kilichofanywa na vijana wa chama cha Mapinduzi kuotesha miti kinapaswa kuigwa na vijana wote pamoja na wadau mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya Nchi.

 


Helena alisema kuwa, watatumia miti hiyo iliyopandwa kuwafundishia wanafunzi kwa vitendo kutunza mazingira kwa kutunza miti hiyo ili iweze kuja kuwafaidisha badae kwa kupata matunda pamoja na kupata kivuli.

 


Aidha alisema kuwa, shule hiyo kwa sasa inauhitaji mkubwa wa miti na kutumia nafasi hiyo kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza shuleni hapo kupanda miti ili kuboresha mazingira ya shule hiyo na kuahidi kupitia wanafunzi miti hiyo itatunza kwa umakini mkubwa.

 

Mwisho….

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI