Header Ads Widget

MWENYEKITI IVAN MOSHI "NI AIBU KWA HALMASHAURI KUSEMA FEDHA ZA MIKOPO YA MAKUNDI MAALUM ZIMEBAKI".

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


UMOJA wa vijana wa Chama cha Mapinduzi umesema kuwa ni aibu kwa Halmashauri kusema fedha za mikopo ya makundi maalum ya Vijana, Wakinamama na Walemavu zimebaki wakati vipo vikundi ambavyo vinahitaji mikopo hiyo na havijafikiwa.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Ivani Moshi wakati wa maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi yaliyoathimishwa katika Himo wilayani Moshi yaliyoambatana na kupanda miti katika shule ya Sekondari ya Himo na badae mkutano wa hadhara.



Moshi alisema kuwa, ni jukumu la watumishi wa Halmashauri kupita vijijini kuwashawishi vijana, kinamama na watu wenyeulemavu kuunda vikundi na kuomba mikopo inayotolewa ili kunufaika na fedha za serikali.



"Ni aibu mtumishi wa Serikali unasimama na kusema fedha za makundi maalum zimebaki kwa sababu vikundi haviji kuomba kwanini msitoke maofisini na kwenda vijijini kuwafwata na kuwaelimisha jinsi ya kuunda vikundi pamoja na kuwasaidia kuvisajili vikundi hivyo ili muwakopeshe hili ndilo jukumu lenu" alisema Moshi.



Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amewataka vijana wa CCM wanapoenda kufanya mikutano ya hadhara kujibu hoja za wapinzani kwa kueleza nini ambacho Serikali imefanya kwa jamii na kuachana na maneno machafu kwani wananchi wanachohitaji ni matendo na sio maneno.



Aliwataka vijana kuondoa hofu kwani yapo mengi ambapo yamefanywa na Serikali ya awamu ya sita na kuwataka kutembea kifua mbele kwa kutangaza mazuri hayo.



Alisema kuwa, katika kuadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi, UVCCM mkoa wa Kilimanjaro wameamua kuadhimisha kwa kupanda miti lengo likiwa ni kuboresha mazingira kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo jumla ya miti 300 ilipandwa.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima vijana ndio walinzi wa Chama na kuwataka kusimama imara ili kuhakikisha uhaika wa chama unaendelea kuwa imara.



Shirima alisema kuwa, lengo lolote la Chama cha Siasa ni kushika Dola hivyo uvccm wanawajibu wa kuhakikisha CCM inaendelea kushika Dola kwa kuwaeleza wananchi kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na chama hicho.



Naye Mbunge wa viti maalum kupitia kundi la Vijana Taifa, Asia Halamga alisema kuwa, wananchi wanapaswa kutembea kifua mbele kutokana na mambo mkubwa yaliyofanywa na Serikali.



Asia alisema kuwa, wao kama Wabunge wamejipanga kujibu hoja za wapinzani kwa vitendo kwani Serikali ya awamu ya sita imeonyesha dhamira yake kwa vitendo ya kuwatumikia wananchi.



"Wanaccm hatuna sababu ya kuwa wapole kwani wananchi wanataka utatuzi wa changamoto zao ambapo CCM inatekeleza kwa vitendo" alisema Asia.


Aidha Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuvitaka vikundi vya Vijana, Kinamama na watu wenyeulemavu vilivyopewa mikopo ya Halmashauri kurejesha fedha hizo ili ziweze kunufaisha vikundi vingine ambavyo viliomba mikopo lakini havikupata.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI