Header Ads Widget

MBUNGE ANNE KILANGO AANZISHA KAMPENI YA KUISAIDIA SHULE KONGWE YA MSINGI PARANE.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME.


MBUNGE wa Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro, Anne Kilango Malecela ameanzisha kampeni maalum ya kuisaidia shule ya msingi Parane iliyopo kata ya Mpinji kuondokana na matatizo ya uchakavu wa majengo pamoja na uhaba wa madawati.


Akikabidhi madawati yaliyotengenezwa na Mbunge huyo, Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Same kwa niaba ya Mbunge, Mohamed Ifanda alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita imejikita katika kupambana na matatizo ya wananchi.Ifanda alisema kuwa, katika sekta ya Elimu serikali imetoa fedha nyingi katika ujenzi wa majengo mapya ya madarasa pamoja na kuanzisha shule mpya hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuunga mkono juhudi za serikali.



Alisema kuwa zipo shule ambazo ni za muda mrefu ambapo majengo pamoja na madawati yamechakaa ambapo Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango ameamua kuanzisha kampeni ya kusaidia shule hizo.


“Mbunge wetu ameamua kutuonyesha njia katika kupambana na matatizo ambayo yanazikabili shule zetu za msingi na sekondari sasa ni jukumu letu sisi wananchi na wapenda maendeleo kumuunga mkono kwa kuchangia madawati pamoja na kujitolea kukarabati majengo ambayo ni chakavu” alisema Ifanda.



Aidha Katibu Mwenezi huyo alitumia nafasi hiyo kuwasihi Wanachama wa Chama cha Mapinduzi kuwaacha Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutekeleza wajibu wao ikiwamo ahadi zao walizotoa mwaka 2020 kwani muda wa kuanza kampeni na muda wa uchaguzi sio sasa.


Awali akisoma risala ya shule kwa Mbunge Anne Kilango, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Parane, Zainabu Chalinga alisema kuwa,shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa madawati hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kukaa chini.



Zainabu alisema kuwa, shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 327 lakini inawalimu 5 hivyo kunauhitaji mkubwa wa walimu pamoja na majengo yake kuchakaa kutokana na kuanzishwa mwaka 1951 na kupelekea miundombinu kuchakaa.Alisema kuwa, wanafunzi hao wanapokuwa shuleni hawasomi kwa amani kutokana na mazingira kutokuwa rafiki kwao.


“Yapo madarasa hayana sakafu ya chini lakini pia kuta zimeweka nyuva huku pia wanafunzi wamekuwa wakilazimika kusoma wakiwa wamekaa chini kutokana na kuwa na uhaba wa madawati na pia tunauhitaji wa walimu watano” alisema Mwalimu Zainabu.



Naye Diwani wa kata ya Mpinji, Namkunda Izungo alisema kuwa, wanafunzi katika shule hiyo ya Parane wamekuwa wakisoma kwa tabu kutokana na kukaa chini hivyo kitendo cha Mbunge Anne Kilango kuanzisha kampeni ya kuisaidia shule hiyo kwa kuchangia madawati itasaidia kuongeza motisha kwa Wanafunzi kusoma.



Namkunda alisema kuwa, kata hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme  ambapo kipo kijiji cha Kirongwe pamoja na vitongoji viwili vya Sambweni havijafikiwa na umeme kabisa.


Mwisho……

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI