Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe LAUTERI KANONI alitoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wanging’ombe kuanza kutenga bajeti ya fedha zitakazowezesha kumalizia ujenzi wa majengo ya nje ya kutoa huduma za matibabu kwa wananchi (OPD) katika vituo vya afya na maboma mengine yaliyokwama.
Hii imetajwa kwenda kuleta tija na ari ya wananchi ya kutoa nguvu zao wanapotakiwa kushiriki kwenye maendeleo kwani kitendo cha kutokamilisha ujenzi wa majengo mbalimbali kwa muda mrefu kunawakatisha tamaa wananchi kuendelea kuchangia shughuli nyingine za maendeleo.
Hayo ameyasema wakati alipokuwa akizindua rasmi kituo cha Afya cha Makoga wilayani Wanging’ombe kwa niaba ya vituo vingine vya Afya vya Ilembula, Saja na Usuka vilivyokamilika kwa gharama ya shilingi milioni mia tano kila kimoja ili kuanza kutoa huduma za matibabu kwa wananchi.
Awali Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Makoga, JAPHET MBWILA akisoma taarifa ya fedha kiasi cha shilingi milioni mia tano zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya kuondoa changamoto ya ukosefu wa kituo cha afya kwenye kata hiyo amesema sasa wananchi wanaanza kupata huduma za afya.
MARIAM MUHAJI ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Wanging'ombe ambaye anakiri kukamilika kwa vituo vinne vya afya hadi sasa.
Diwani wa Kata ya Makoga, JAIROS LUNYUNGU alimuomba mkuu huyo wa wilaya kuendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye kituo hicho huku wananchi akiwemo SIKUJUA MGINA wakimshukuru Rais DOKTA SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuwajengea kituo hicho.
Ujenzi wa vituo vya afya katika kata mbalimbali hapa nchini unakwenda kupunguza changamoto za afya kwa wananchi ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufanya safari kwenda kutafuta huduma hizo.
0 Comments