Na Amon Mtega, Madaba.
WAKAZI wa Kata ya Lituta Jimbo la Madaba Mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Jimbo la Madaba Dkt Joseph Mhagama kwa kujenga shule ya Sekondari katika Kijiji cha Kipingo kilichopo katika kata hiyo kwa lengo la kuwapunguzia adha wanafunzi waliyokuwa wakienda shule umbali mrefu.
Akizungumza mmoja wa wakazi wa kata hiyo Michael Lugongo amesema kuwa shule hiyo iliyojengwa kwa fedha za Serikali bila mchango wa Wananchi itasaidia kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikiwapata wanafunzi hasa wanafunzi wa kike katika upataji mimba kutokana na kwenda kusoma umbali mrefu jambo ambalo limekuwa likiwafanya wakutane na vishawishi.
Lugongo amesema kuwa katika kipindi cha nyuma baadhi ya wanafunzi wa kata hiyo walishindwa kuhitimu elimu yao ni kutokana na utoro na upataji mimba hivyo kwa sasa wanaamini kuwa tatizo litapungua kwa kuwa shule hiyo ipo katika eneo lao jambo litakalo saidia mwanafunzi kupunguza utoro.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Madaba Dkt Joseph Mhagama amesema kuwa ujenzi wa Sekondari hiyo ni fedha iliyotolewa na Serikali ya awamu ya sita inayongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutaka ijenge shule sehemu yenye changamoto ili kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Mbunge Dkt Mhagama ambaye anapita kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali kwenye Jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa shule hiyo ambayo Wananchi wameamua kuipatia jina la sekondari ya Dkt Joseph Kizito Mhagama ikiwa ni sehemu ya kujali mchango wake katika kuuendeleza jimbo hilo amesema kuwa miradi mbalimbali itaendelea kutekelezwa .
0 Comments