Header Ads Widget

VIJANA MOSHI VIJIJINI WATAKIWA KUJIKWAMUA KIUCHUMI KUPITIA KILIMO...

Na Gift Mongi, MATUKIO DAIMA APP, MOSHI

Vijana katika wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wametakiwa kujikwamua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zinazowazunguka ikiwemo kilimo ili kuweza kujikwamua kiuchumi badala ya kuishi Kwa ndoto za kusubiria ajira pekee.


Hii inatokana na Moshi kuwa eneo kubwa linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo vijana wakijiunga katika vikundi wanaweza kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo ambayo ni tegemezi kwenye maisha ya kila siku ya mwanadamu.


Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM)wilaya ya Moshi Vijijini Yuvenail Shirima ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi ofisi ya katibu wa umoja huo kata ya Kirua Vunjo Kusini mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa wilaya.


Katika hafla hiyo ambayo pia amekabidhi vifaa vya mziki vyenye thamani ya zaidi ya milioni tano  kwa umoja huo ngazi ya kata kama kitega uchumi amesema vijana walio wengi kwa sasa wanaonekana kusuasua katika suala la kujikwamua  kiuchumi jambo linalokwamisha maendeleo.


"Siasa zinaenda na uchumi imara hivyo ni lazima vijana tuhakikishe tunaenda kujikwamua kiuchumi na uzuri hapa Moshi tuna maeneo makubwa yanayofaa kwa kilimo tujipange tuchangamkie fursa hii tusiishi kwa kulalamika pekee"amesema

Amesema serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira rafiki katika kuwainua vijana ikiwemo mikopo isiyo na riba kutoka katika halmashauri na kuwa kama wataenda kujiunga itawawia rahisi kuweza kunufaika na mikopo  hiyo hivyo suala la mitaji litakuwa limeshapatiwa ufumbuzi tayari.


"Mikopo hii ipo tena ni mahususi kwetu sisi vijana natamani sana tukikutana hapa siku nyingine kila kijana awe tayari ana mradi uliosimama na tusiishi kwa kulalamika pekee kuwa ajira hakuna lazima tuonyeshe njia lakini pia na uthubutu"anasema


Hata hivyo Shirima amekemea tabia ya maafisa maendeleo katika kata ambao wataleta urasimu au kuonyesha kukwamisha vijana hao kutonufaika na mikopo hiyo kwani kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu jitihada za serikali kuwainua vijana 


"Natoa agizo hapa leo ikionekana kuna mtu anakwamisha vijana msipate hii mikopo sisi tunamwesabia kama mkwamisha maendeleo na tutashughulika naye mazima katika hili hakuna ubishi"anasema


Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM)kata ya Kirua Vunjo Kusini Proches Njau ameshukukuru kwa kukabidhiwa vifaa hivyo na kuahidi kuvitumia vyema kwa ustawi wa jumuiya hiyo.

Aidha ameshukuru pia kukabidhiwa ofisi mpya iliyokarabatiwa ya umoja huo kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo na kuwa kwa sasa umoja huo unaenda kuwa moja ya vijana wa kuigwa katika uendeshwaji wake kwa kuwa na mambo yaliyonyooka.


"Sina chakusema kwa leo ila nashukuru mwenyekiti kwa kutekeleza ahadi yako ya kutupa vyombo vya mziki lakini pia ofisi yetu mpya niwaahidi vijana hii ni mali yetu tubitumie vyema kwa ustawi wa jumuiya yetu hii"amesema


Merikiyori Pantaleo ni katibu wa UVCCM wilaya ya Moshi Vijijini ambapo amesema vijana kwa sasa sio watu wa kupelekeshwa kama kipindi cha nyuma na kuwa  jitihada mbalimbali zinazofanyika za kuleta maendeleo hakuna mtu asiyeziona.


"Shule zinajengwa,zahanati miradi ya maji pia sasa hakuna kijana atakayeyumbishwa tena hao wa upande wa pili wabaki tu wamenyoosha vidole na sisi tunyooshe maendeleo alafu tukutane kwenye uchaguzi 2024 na 2025"amesema

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS