Na Amon Mtega _Namtumbo.
MICHUANO ya Kombe la Mantra yaliyoandaliwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Vita Kawawa ambayo yameshirikisha timu 14 kutoka kwenye kata zote za Jimbo hilo yamekamilika kwa timu ya Rwinga kuibuka mshindi dhidi ya timu ya Lusenti ambao wameibuka mshindi wa pili katika ligi ya mtoano
Akizungumzia mashindano Mratibu wa mashindano ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Namtumbo(Nadifa) Zuberi Kossa amesema kuwa Mshindi wa mashindano hayo ni timu ya Rwinga ambayo imejinyakulia zawadi ya kombe, fedha taslimu laki sita, na mpira mmoja, pia mshindi wa pili ambaye ni Lusenti imejipatia zawadi ya shilingi laki nne na mpira mmoja.
Kossa ameeleza kuwa pia mshindi wa tatu amejinyakulia zawadi ya shilingi laki mbili na mpira mmoja na kwamba zawadi nyingine ambazo zimetolewa na mdhamini wa mashindano hayo ni kwa mchezaji bora, kipa bora , kocha bora na timu yenye nidhamu kwa kila kipengele imetolewa shilingi elfu kumi
Mratibu huyo amefafanua kuwa mashindano hayo yalishirikisha timu kutoka kata 14 za Kitanda, Mchomoro,Luegu,Luchili,Mputa,Ligera,Namtumbo, Mgombasi,Likuyu,Rwinga, ambapo kila timu iliyoshiriki walipewa jezi seti moja na mdhamini.
Kossa amesema kuwa wanamuomba mdhamini na wadau wengine wa michezo waweze kuboresha mashindano hayo ili yaweze kuleta furaha na tija kwa wadau wote kuwa ni Pamoja na mashindano hayo yaanze mwezi juni na kumalizika mwezi septemba kwa kuzingatia jiografia ya Jimbo hilo.
Hata hivyo amependekeza kuwa mashindano hayo yaanzie katika ngazi ya vilabu kwenye vijiji na kupanda katika ngazi zingine, kuleta wataalamu wa michezo ili kuwafundisha wataalamu watakaosaidia kuinua viwango vya michezo, Pamoja na kuwasaidia seti za jezi waamuzi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa amesema kuwa mashindano hayo yalianzishwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi na wakazi wa Namtumbo kwa mambo mbalimbali kama vile elimu,afya,maji,watu wenye mahitaji maalumu,michezo na utamaduni,madaraja na barabara na elimu ya usalama barabarani.
Kawawa akiwa uwanjani hapo amesema kuwa wananchi wanatakiwa waunge mkono jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali ikiwemo kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita pamoja na kampuni ya Mantra katika sekta zote ili kuifanya Namtumbo isonge mbele kwa maendeleo ya Wananchi.
Akikabidhi zawadi kwa washindi katika mashindano ya mwaka 2022 Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu amesema kuwa mashindano hayo yamefanikiwa vizuri kutokana na kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayomiliki madini ya Urani katika Wilaya hiyo pamoja na Mbunge wa Namtumbo kutoa udhamini jambo ambalo limeongeza hamasa ya kutafuta namna ya kuanzisha timu ya Wilaya kwa siku za mbele.
Mkuu huyo ambaye ameipongeza kampuni ya Mantra na Mbunge wa Namtumbo kwa udhamini huo amesema kuwa ofisi yake inafanya kila mbinu ya kuhakikisha inakuwa na timu ya Wilaya ambayo itakayokuwa inaleta ushindani na timu zingine zikiwemo za Nje ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Meneja uhusiano wa Kampuni ya Mantra Khadija Kawawa amesema kuwa kampuni hiyo imetoa udhamini wa fedha, kombe, na jezi ambazo timu zote 14 zilipatiwa jezi.
Kawawa amesema kuwa Kampuni ya Mantra imekuwa ikidhamini mashindano hayo kila mwaka, pia imekuwa ikijikita kwenye shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii ambayo inaiyo wazunguka.
0 Comments