Header Ads Widget

TAHEA WAZINDUA JARIDA LA MBELEKO LITAKALOWASADIA WAZAZI KATIKA SUALA LA MAKUZI NA MALEZI KWA WATOTO

 

Afisa ustawi wa jamii Mkuu Wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Loata Mollel.

Mkurugenzi kutoka shirika la TAHEA Mary Kabati
Peter Matyoko mratibu wa mradi ya elimu kutoka TAHEA

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

NA CHAUSIKU SAID,MATUKIO DAIMAAPP MWANZA.

Shirika la uchumi wa Nyumbani (TAHEA) Mkoa wa Mwanza limezindua Jarida la Mbeleko litakalosaidia kutoa elimu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla juu ya malezi bora kwa watoto ili waweze kukua katika maadili mazuri na kuwa raia wema.


Uzinduzi huo ulifanyika katika  Kituo cha malezi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kata ya  Bugogwa Mtaa wa Igombe Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza.


Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Jarida hilo Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Loata Mollel, amesema jamii inapaswa kuwekeza nguvu nyingi katika malezi na makuzi ya watoto kwani kwakufanya hivyo itawasaidia kukua vizuri na kutimiza ndoto zao.


" Wazazi,walezi muda mwingi wameuwekeza kwenye utafutaji wa ridhiki kwenye suala la  malezi ya watoto wamewaachia  wafanyakazi wa nyumbani, nawasihi wazazi kuweka ratiba ya kusoma majarida mbalimbali yanayohusu malezi ya watoto likiwemo la Mbeleko ili waweze kuwalea watoto vizuri na kuwajengea misingi bora", amesema Mollel 


Ameeleza kuwa Sayansi na Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa katika kujua mambo mbalimbali lakini pia imeleta changamoto kwenye malezi ya watoto kutokana na vitu vinavyokuwa vikioneshwa kwenye runinga hivyo wazazi wanatakiwa kuwa makini ili kuweza kuwanusuru watoto wao.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la TAHEA Mwanza Mary Kabati, amesema lengo la kuzindua jarida hilo ni kuendelea kuhamasisha jamii kuweka mazingira rafiki kwa watoto hususani kwenye malezi.


Amesema suala la malezi kwa watoto ni la muhimu sana lakini wazazi wengi hawana nafasi ya kukaa na watoto wao wala kujua maendeleo yao ya kimasomo.


" Ninaimani kupitia Jarida hili la MBELEKO wazazi na walezi watapata muongozo mzuri wa kuwalea watoto wao kwa kufahamu changamoto mbalimbali zinazoweza kuwapata pindi wanapokosa malezi bora", ameeleza Kabati


Peter Matyoko ni mratibu wa miradi ya elimu kutoka Shirika hilo amesema, Jarida hilo linatumia mifano halisi ya utoaji malezi inayoonekana katika familia na jamii na kujaribu kukosoa,kusisitiza na kuboresha malezi hayo kwakutumia simulizi ambazo zimetoka kwa watu mbalimbali.


Ameeleza Jarida hilo limetumia vibonzo katika kuonyesha matukio yanayojitokeza katika familia na mitaani yanayohusiana na malezi ya watoto ili kuweza kufikisha ujumbe,kuongeza radha, na kuwavutia wasomaji pia linatoa fursa kwa wazazi, walezi na jamii nzima kujadili na kutafakari juu ya malezi ya watoto kwa wakati huu ili kuchochea mabadiliko.


Anamaria Mwenge na Pastory Mswanzali ni miongoni mwa wazazi waliohudhuria uzinduzi huo wamesema, Jarida la Mbeleko litawasaidia kujua mbinu mbalimbali za kuwalea watoto.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS