Header Ads Widget

MBUNGE ATAKA UTEKELEZAJI MIRADI UBADILISHE MAISHA YA WANANCHI.

Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru (katikati Mwenye suti) akiongoza viongozi wa CCM na serikali ya kata ya Janda wilaya ya Buhigwe akikagua daraja la Mto Luiche ambalo ni moja ya madaraja ya mawe yanayojengwa wilayani humo kurahisisha shughuli za usafirishaji maeneo ya kilimo.

Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru (katikati Mwenye suti) akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Janda wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.


Mkuu wa polisi kata ya Janda wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Inspekta Chris Chrisant Geroge (kulia) akitoa maelezo kwa Mbunge wa jimbo la Buhigwe Felix Kavejuru (wa tatu kulia) kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha polisi kwenye kata hiyo wakati mbunge na viongozi wa CCM walipotembea kuona maendeleo ya mradi huo ambapo Mbunge ameahidi kutoa shilingi milioni tano za bati zinazohitajika kukamilisha mradi huo.


(Picha na Fadhili Abdallah)

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MBUNGE wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru amewataka wananchi wa jimbo hilo kutumia mpango wa kuboresha miundo mbinu mbalimbali ya jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na madaraja kama fursa kwao kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Kavejuru alisema hayo alipofanya ukaguzi kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye jimbo hilo ikiwemo miradi ya madaraja ya mawe kwenda kwenye eneo la mashamba ya wananchi.

Mbunge huyo alisema kuwa kwa sasa miradi 40 inatekelezwa kwenye jimbo hilo ikiwemo miradi ya maji, elimu,afya,kilimo na barabara ambapo kwenye miradi ya barabara zipo barabara chini ya TARURA,TANROADS na miradi mikubwa ya kitaifa ambapo yote imelenga kubadilisha hali za kiuchumi za maisha ya wananchi wa jimbo hilo.

Akiwa kwenye baadhi ya madaraja ya mawe yanayojengwa na TARURA mbunge huyo alisema kuwa yana maana kubwa katika kuimarisha shughuli za kilimo ambazo ndiyo shughuli kuu za wananchi wa jimbo hilo kwa kuwezesha wananchi kupita kwa urahisi kwenda mashambani lakini pia urahisi wa kusafirisha mazao yao kutoa mashambani kwenda kwenye masoko.

Diwani wa kata ya Janda, Stanley Ndoza ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa ujenzi wa madaraja hayo ya mawe ambayo yamewakomboa sana wakulima kwa kuweza kwenda shamba na kurudi sambamba na kuweza kusafirisha mazao kwa urahisi.

Ndoza alisema kuwa wakati wa masika baadhi ya mito ilikuwa haipitiki na iliwalazimu baadhi ya watu kulala mashambani au kupitia njia ndefu za mzunguko kutokana na mito kujaa ambayo mingine madaraja ya muda waliyokuwa wakijengwa yalikuwa yakibebwa na maji.

Mmoja wa wananchi wa kata ya Janda, Yoram Binza alisema kuwa miradi inayotekelezwa kwenye jimbo hilo imekuwa chachu kubwa kiuchumi ikiwemo madaraja ya mawe ambayo yamefungua njia za usafirishaji kuingia na kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hilo wakati wote ambapo wakati wa mvua ilikuwa changamoto kubwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS