Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Philip Mpango amesema wapo baadhi ya viongozi ambao kwa maslahi yao binafsi
wanachangia uharibifu wa mazingira na kwamba haamini kama kuna maskini mwenye
uwezo wa kuingia katika vyanzo vya maji akiwa na zaidi ya mifugo 3000
Dkt. Mpango, amesema hayo leo Desemba 19, 2022
katika Kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi, Mazingira na Utunzaji wa
vyanzo vya maji, na kusema viongozi wa namna hiyo hawafai kwa kuwa wanaweka
rehani maisha ya watanzania na kwamba Serikali haiwezekani kuacha tabia hiyo
iendelee kwakuwa ina madhara kwa jamii.
Awali, Mwenyekiti wa jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Deodatus Balile, alipopata nafasi ya kuzungumza alisema yupo tayari kutoa
majina ambayo ni familia 12 zinajimilikisha eneo katika bonde la Usangu kinyume
cha sheria na kupelekea maeneo mengine kukosa maji.
Balile amedai ndani ya familia hizo wamo baadhi ya wabunge,
majaji, mawaziri na baadhi ya viongozi wengine wa serikali.
Mwenyekiti wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na
Taarifa MECIRA, Habibu Mchange amesema kuwa shughuli za kibinadamu zinazofanywa
na wananchi wachache katika bonde la Ihefu ndio wamekuwa chanzo cha kukauka kwa
Mto Ruaha.
Mchange amesema, kutokana na uharibifu huo kumepelekea wanyama
wengi katika hifadhi ya Taifa Ruaha kufa na wengine kuambukizwa magonjwa
mbalimbali kutokana na kukosa maji ya kutosha.
0 Comments