NA WILLIUM PAUL, SAME.
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa michezo ikitumika vizuri itasaidia kuondoa makundi yasiyofaa katika jamii na kupunguza wahalifu.
Ridhiwani alitoa kauli hiyo jana wakati wa fainali ya mashindano ya Anne Kilango cup tarafa ya Ndungu wilayani Same mkoani Kilimanjaro yaliyozikutanisha timu ya Bodaboda kutoka kata ya Kihurio na Kizerui kutoka kata ya Maoreyaliyothaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela.
Kikwete alisema kuwa, endapo kutakuwepo na nidhamu katika michezo vijana wote watakuwa na nidhamu na kupelekea kutojiunga katika makundi yasiyofaa katika jamii na kufanya uhalifu.
“Michezo inawafanya vijana kuwa bize hizo hawatapata muda wa kujiunga katika makundi maovu na kufanya uhalifu badala yake watakuwa mstari wa mbele kuwafichua wahalifu ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria” alisema Kikwete.
Aidha alisema kuwa ipo haja ya kuwa na walimu wa kufundisha michezo katika jimbo la Same mashariki ambapo aliahidi kupeleka mwalimu wa kuwafundisha vijana mpira.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela alitumia nafasi hiyo kuwasihi vijana kulinda amani iliyopo nchini kwani ipo kwa ajili ya vijana.
Alisema kuwa, tangu nchi za bara la Afrika zipate Uhuru ni nchi moja pekee imeendelea kulinda amani yake ambayo ni Tanzania na kuwataka vijana kuendelea kuilinda na kuepuka kutumika kuivuruga amani hiyo.
“Nimpongeze Mbunge Anne kwa kuona umuhimu wa kuwakutanisha vijana wa jimbo lake kwa kuanzisha michezo na ninyi vijana tumieni mpira huu kujenga undugu, ushirikiano na mshikamano ili kuhakikisha mnajiletea maendeleo yenu”alisema Malecela.
Naye mdhamini wa mashindano hayo, Anne Kilango alisema kuwa, mashindano hayo katika tarafa ya Ndungu yalishirikisha timu 34 lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani katika kuinua michezo.
Alisema kuwa, mashindano hayo ambayo yalianza kwa tarafa ya Miamba na badae tarafa ya Gonja na kuhitimishwa na tarafa ya Ndungu ambapo mshindi wa kwanza wa kila tarafa alijishindia fedha taslimu milioni 1, medali pamoja na kombe huku mshindi wa pili akijinyakulia laki nane pamoja na medali na mshindi wa tatu laki sita pamoja na medali.
Katika fainali hiyo timu ya Bodaboda iliibuka kidedea kwa mikwaju ya penati 5 kwa nne dhidi ya Kizerui baada ya dakika 120 kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili.
Mwisho…
0 Comments