NA WILLIUM PAUL, SAME.
MBUNGE wa Viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amewataka wakinamama kutowafumbia macho wale wote wanaofanya ukatili dhidi ya watoto na wanawake kwani kufanya hivyo ni kuharibu kizazi cha badae.
Zuena ametoa kauli hiyo jana alipokutana na Wajunbe a Mkutano mkuu wa Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), wilaya za Same na Mwanga ambapo alisema kuwa, matendo ya ukatili yamekuwa yakiongezeka kila wakati.
Alisema kuwa, wakinamama ni jeshi kubwa na ndio wenye uchungu na watoto na kuwawataka kila mmoja kujenga urafiki na watoto wa kike na kiume ili waweze kuwaeleza yale wanayofanyiwa na kuweza kuwafichua wahusika ili kukomesha matukio hayo.
“Huko nyuma tulikuwa tukisikia watoto wa kike pekee ndio walikuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia lakini kwa sasa hata watoto wa kiume nao wamekuwa wakifanyiwa ukatili huo sasa tukiyafumbia macho matukio haya sijui tutakuwa tunatengeneza kizazi gani hapa tuunganeni kupinga matukio haya” alisema Zuena.
Mbunge huyo alitaka jamii ifike mahali na kukataa matuiko hayo ya ukatili na kuiomba kuungana na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kupambana na matukio ya ukatili.
Aidha Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaondoa hofu wakinamama pindi watakapowafichua watu hao maisha yao kuwa rehani na kudai kuwa serikali itamlinda mtoa taarifa ya wale wote wanaowafanyia ukatili watoto na wanawake.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo, aliwasisitiza wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni kwani wapo watoto ambao wamekuwa hawafiki shule na kujiunga katika makundi yasiyofaa katika jamii.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sasa ni jukumu letu sisi wazazi kuhakikisha watoto wetu wanasoma na ili kujua hili ni lazima kufuatilia maendeleo ya watoto shule pamoja na kujenga ukaribu na walimu” alisema Zuena.
Mwisho
0 Comments