Na Gift Mongi, MATUKIO DAIMA APP, Moshi.
Wananchi wapatao 13,734 katika kata ya Njiapanda halmashauri ya Moshi wanaenda kuondokana na mgao wa maji uliokuwa ukiwakabili baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Miwaleni-Njiapanda.
Shilingi bilioni 2.378 zimetumika hadi kukamilika kwa mradi huo ikiwa ni fedha kutoka serikalini ambapo hadi sasa umeshakamilika kwa asilimia 99 kwa mujibu wa msimamizi wa mradi huo ambaye ni Mamlaka ya majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).
Akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi(CCM)mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi mkurugenzi mtendaji wa MUWSA,mhandisi Kija Limbe alisema mradi huo ni moja ya ahadi za serikali kwa wananchi hao na kuwa utaenda kumaliza kero iliyodumu kwa kipindi kirefu.
Alisema mpaka sasa serikali imeshatoa Sh 2.376 bilioni, kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambao una uwezo wa kuhudumia kata ya Njiapanda na maeneo jirani na unaenda kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na kwa siku 10 zijazo utakuwa umekamilika.
"Mwenyekiti huu mradi tunautekeleza sisi wenyewe kama ambavyo unauona na ni fahari yetu kama MUWSA kuona miradi ya maji inatekelezwa kama ilivyopangwa kwani ni dira ya serikali kumtua mama ndio kichwani"alisema mhandisi Limbe
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi alisema kuwa mamlaka hiyo imeendana na kasi ya rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo suala la maji na kuwa miradi ya kimkakati inatakiwa iende kwa viwango na thamani ya hela ionekane kama ilivyo kwa mradi huo
Aidha alisema mradi huo kukamilika kwake kutaenda kuongeza ufanisi wa shughuli mbali mbali lakini pia kuchangia kukua kwa shughuli za uzalishaji tofauti na ilivyokuwa watu kutumia muda mwingi kutafuta maji na kusimamisha shughuli za kimaendeleo.
"Niwashukuru sana sana kwa kusimamia na kutekeleza ilani kwa vitendo hii ndio aina ya ufanisi ambayo CCM na serikali tunayoiongoza tunaitaka maana tuliahidi na sasa tunautekeleza na tena kwa viwango"alisema Boisafi
Mbunge wa Vunjo Dkt Charles Kimei aliishukuru serikali kwa namna ilivyotoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ambavyo wananchi waliahidiwa na chama cha mapinduzi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Alisema mradi huo umejengwa kwa kiwango lakini pia ndani ya wakati ambapo MUWSA wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana katika kutekeleza ahadi hiyo na kuwa siku chache zijazo wananchi wataanza kunufaika na mradi huo kwa kupata maji ya ukakika.
0 Comments