NA MWANDISHI WETU, MATUKIODAIMA App Dar
KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kuweka wazi ratiba ya utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kuhusu masuala ya demokrasia nchini ili kurudisha imani kwa wananchi na kupunguza malalamiko katika masuala ya siasa nchini.
Mbali na hilo Zitto pia ametoa ushauri wa utatuzi wa masuala sita waliyoyabaini katika ziara yake kwenye mikoa mitatu ya Kusini ambayo ni Selous, Mtwara na Lindi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Zitto alisema suala la utawala bora linapaswa kuzingatiwa kwani kumekuwapo na vitisho dhidi ya wananchi wanapotekeleza haki zao za kisiasa.
Alisema vitisho dhidi ya wananchi amekutana nalo katika Wilaya ya Tunduru na Ruangwa walipokuwa kwenye ziara hiyo.
"ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iweke wazi ratiba ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu masuala ya demokrasia nchini.
"Mapendekezo haya yakitekelezwa yatarejesha imani ya wananchi katika mfumo wa demokrasia nchini na kupunguza malalamiko na nyongo za wananchi kwa kiasi kikubwa,"alisema Zitto.
Aidha alisema wananchi bado wanalalamikia matendo ya wagombea wa vyama vya upinzani kutekwa bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya watekaji.
"Mfano ambao umerejewa sana ni mgombea wa Jimbo la Ruangwa kutoka ACT Wazalendo mwaka 2020 ambaye alitekwa na kutupwa msituni Mkuranga mkoani Pwani.
"Hakuna uchunguzi wowote umefanyika mpaka sasa. ACT Wazalendo tunaendelea kutoa wito kwa Serikali kujenga mahusiano mema na wanasiasa wa upinzani kwani nchi hii ni ya kidemokrasia, sio nchi ya chama kimoja na upinzani sio uadui,"alisema Zitto.
Zitto alishauri viongozi wa kitaifa wawe mfano bora wa kuheshimu demokrasia katika maeneo wanayotoka ili kuwa mfano kwa maeneo mengine.
"Jimbo la Ruangwa ni eneo ambalo wananchi ambao ni wanachama wa vyama vya upinzani wanaishi kwa hofu kubwa sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu inabidi uwe mstari wa mbele kuondoa hofu hii kwa kukaa na viongozi wa vyama vya upinzani katika jimbo hili, kuzungumza yaliyopita na ikibidi kuombana radhi na kujadili kwa pamoja namna ya kusukuma ajenda ya maendeleo ya Ruangwa kwa pamoja,"alisema Zitto.
Mbali na hilo Zitto pia alizungumzia tatizo la migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambalo alidai linaweza kuleta athari kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
"Majimbo yote tuliyopita tumekutana na vilio vya wakulima kuhusu mahusiano yao na wafugaji.,wkulima wanalalamika kuvamiwa na wafugaji kwenye mashamba yao na mifugo hiyo kula mazao ya wakulima.
"Viongozi wa Serikali wakipatiwa taarifa juu ya kadhia hizo hawachukui hatua stahiki kushughulikia matatizo yao, wafugaji wananywesha mifugo yao kwenye vyanzo vya maji vinavyotegemewa na wanakijiji,"alisema Zitto.
Alisema athari za migogoro hiyo imepelekea kuwa na mapigano baina ya wakulima na wafugaji, mapigano yanayohatarisha amani na usalama nchini.
"Tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika Wilaya za Tunduru, Ruangwa, Nachingwea, Liwale, Lindi Vijijini na Kilwa. Mfano kwa Mkoa wa Lindi (Kilwa na Nachingwea) pekee migogoro hiyo ndani ya mwaka mmoja imepelekea vifo vya watu 12, taarifa za watu waliojeruhiwa wanakadiriwa kufikia 36.,"alisema Zitto.
Alisema Nachingwea inakabiliwa na baa la njaa miongoni mwa sababu ni mashamba ya wakulima kuvamiwa na wanyama waharibifu pamoja na mifugo.
Alisema uamuzi wa Serikali kuwaruhusu wafugaji kwenye ardhi ya Kilimo bila kuwashirikisha wanavijiji wenyewe ni kupandikiza mapigano yasiyo ya lazima.
"Tukiwa katika Ziara tulitoa wito kwa Serikali kuchukua hatua kadhaa kumaliza migogoro hiyo, tunaendelea kusisitiza kuwa,kwanza serikali itumie majukwaa rasmi kama Kamati za Mashauriano za Wilaya na Mikoa (RCC na DCC) kujadili masuala haya kwa upana na kuhusisha wawakilishi wa wakulima na wafugaji ili kujenga maelewano miongoni mwao.
"Pili tunapendekeza kuwasikiliza wanavijiji na kuwashirikisha kwenye mipango bora ya matumizi ya ardhi ya vijiji. Na pia, kusimamia utekelezaji wa mpango ulioamuliwa na vijiji vyenyewe bila uonevu wa kundi lolote."alisema Zitto.
Alisema serikali iwawekee wafugaji mazingira mazuri ya kufugia kwa kujenga malambo ya kunyeshea mifugo na kutengea maeneo ya malisho. Utaratibu wa sasa unasabaisha vurugu, wanalisha kwenye mashamba ya wakulima, wananywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinahudumia wanavijiji.
Alisema jambo jingine waliloliona ni Uvamizi wa Tembo kwenye mashamba ya wakulima na makazi ya wananchi.
Maeneo mengine tuliyopita hususani vijiji vinavyozungukwa na hifadhi ya Wanyama pori ya Selous tumepokea malalamiko ya wananchi kutokana na kuibuka kwa kasi kubwa wimbi la uvamizi wa Tembo.
"Tatizo hili limeikumba zaidi jimbo la Tunduru Kusini na Kaskazini, wilaya ya Nachingwea, Ruangwa, Lindi Vijijini, Liwale na Kilwa,uvamizi wa tembo kwenye makazi na mashamba unasababisha hasara kubwa sana kwa kuharibu mazao ya wakulima, wanajeruhi watu, kuharibu makazi na hata kusababisha vifo vya watu,"alisema Zitto.
Alisema taarifa za hivi karibu mathalani wilaya ya Liwale Mkoani Lindi inakabiriwa na janga la njaa kutokana na Tembo kuharibu mazao yao (korosho na mazao ya nafaka).
Sisi ACT Wazalendo mara kadhaa kupitia kwa Katibu Mkuu wa Chama Ndg. Ado Shaibu tulipaza sauti na kuishauri Serikali hatua za kuchukua hususani kuitaka iwajibike kwa kufanya utafiti wa kina ili kujua kwanini kuna Ongezeko kubwa la matukio ya tembo kutoka Mbugani na kuvamia vijiji. Pia, tuliitaka Serikali kuongeza uwezo wa kudhibiti matukio hayo kupitia idara ya wanyapori,"alisema Zitto.
Alisema wanaendelea kusisitiza kwa kuitaka Serikali iwajibike kwa kuongeza idadi ya askari wanyamapori hususani wakati wa kilimo na mavuno angalau kila Kijiji chenye uvamizi wa mara kwa mara kuna kuwa na askari.
Pia, wameitaka Serikali itoe fidia (vifuta jasho na machozi) za uharibifu unaofanywa na wanayama hao kwakuzingatia hali halisi za gharama za maisha na uharibifu.
Alisema siala jingine ni kushuka kwa bei ya korosho na mfumo wa stakabadhi ghalani
Wananchi wengi ambao wanategemea korosho kama uti wa mgongo wa uchumi wao wamelalamikia kuporomoka kwa bei ya Korosho.
"Minada yote iliyotangazwa haizidi Shilingi 2100 kwa kila Kilo moja,wananchi wengi wanalalamika kuwa bei katika minada zinapangwa na hivyo kuufanya mfumo wa stakabadhi ghalani kutokuwa na msaada kwao.
Aidha, kuna kilio cha wananchi juu ya kutoridhishwa na mfumo wa stakabadhi ghalani,wakulima wanalalamikia kucheleweshewa malipo yao wakiuza mazao wanasubiri malipo wiki mbili kwa kuwahi lakini hadi miezi mitatu kwa baadhi ya maeneo,"alisema Zitto.
0 Comments