Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Nape Nnauye amesema hakutakuwa na mabadiliko ya bei za bando yoyote
hadi tathmini ya gharama itakapokamilika.
Tathmini
hiyo inayofanywa kila baada ya miaka mitano, inatarajiwa kukamilika kati ya
Desemba 2022 hadi Januari 2023.
Ameyasema
hayo leo Jumatatu, Novemba 21, 2022 wakati wa mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika makao makuu ya ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
jijini Dar es Salaam.
Nape
amesema kwa sasa watoa huduma wote wako katika viwango vya bei elekezi
iliyowekwa na Serikali ambayo ni kati ya Sh2.03 hadi Sh9.35.
"Hatutegemei
mabadiliko yoyote kwa kipindi hiki hadi tathmini itakapokamilika, niwaombe
wananchi wasione hatuhangaiki na suala hili, tumekuwa tukihangaika nalo."
"Sasa
tumefikia hatua ambayo tumesema tutatulia hadi tathmini itakapokamilika na
matumaini yetu kuwa itatupa muelekeo mzuri," amesema Nnauye
Hiyo ni
kutokana na kile alichokieleza tathmini itaelezea uwekezaji uliofanyika, hatua
za kikodi zilizochukuliwa, marekebisho yaliyofanyika na itatoa matokeo kuwa
gharama zinaweza kushuka kwa kiasi gani.
"Lakini
wakati tukisubiri matokeo ya tathmini hiyo hakutakuwa na mabadiliko na
tumewataka TCRA kwani wanapaswa kupelekewa maombi ya mabadiliko kuwa kwa sasa
watulize sekta watu waendelee kutumia huduma," amesema
Hili
linafanyika ikiwa ni muendelezo wa ushughulikiaji malalamiko ya wananchi juu ya
upandaji holela wa vifurushi unaofanywa na mitandao ya simu jambo ambalo
limekuwa likifanya vilio kusikika kila kona.
Malalamiko
hayo yamekuwa yakijikita zaidi katika bando la intaneti, kwa mfano mtandao
mmoja nchini umebadilisha bei za kifurushi cha data kilichouzwa kwa Sh1,000
awali kiliwezesha megabaiti 450 kwa wiki, lakini sasa kwa bei hiyo zinapatikana
megabaiti 350 sawa na upungufu wa asilimia 10.
Pia,
kifurushi cha Sh 20,000 kilichokuwa kikitoa gigabaiti 12 kwa siku 30 hivi sasa
kinatoa gigabaiti 9.5 kwa siku 30. Sh2, 000 iliyokuwa ikinunua gigabaiti 1.1
kwa siku tatu hivi sasa inanunua megabaiti 985.
0 Comments