NA CHAUSIKU SAID,MATUKIO DAIMAAPP MWANZA.
Waandishi wa habari kutoka Kanda ya ziwa wamepewa mafunzo juu ya magonjwa yasiyoambukiza ili waweze kuandika na kuripoti habari zitakazoleta tija kwenye jamii .
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya afya Shadrack Buswelu, alipokuwa akizungumza kwenye semina iliyofanyika Jijini Mwanza na kusema kuwa lengo la kuaandaa mafunzo hayo ni kuwawezesha waandishi wa habari kutoa taarifa ambazo ni sahihi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza kwenye jamii ili waweze kuchukua hatua madhubuti ya kujikinga.
Buswelu ameeleza kuwa waandishi wa habari wataendelea kuelimisha jamii Kwa kufikisha taarifa sahihi kuhusiana na Kinga ya magonjwa yasiyoambukiza.
"Nina Imani wataweza kuelezea viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo matumizi makubwa ya pombe,lishe, kufanya mazoezi pamoja na kupunguza matumizi ya tumbaku" Alisema Buswelu.
Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Andrew Swai, amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaenea kwa wingi ikiwemo kisukari, Saratani,magonjwa sugu ya njia ya hewa,kuoza meno, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, na magonjwa ya akili.
"Tafiti za Mwaka 2012 zilizofanyika Tanzania nzima katika Wilaya 50 ugonjwa wa kisukari uliongezeka na kufikia asilimia 9 msukumo wa juu wa damu ulifikia asilimia 26 unene uliozidi ulifikia asilimia 34, kwa sasa Dunia nzima asilimia 71 ya vifo vyote vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza na kwa Tanzania asilimia 34 ya vifo vinatokana na magonjwa hayo", amesema Prof. Swai
Amesema sababu za kuongezeka kwa magonjwa hayo ni mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi,ulaji usiofaa,matumizi ya pombe,tumbaku na madawa ya kulevya,utawala duni wa msongo wa mawazo,kutopata usingizi wa kutosha,ajali au matukio yenye kusababisha majeraha mwilini pamoja na matukio ya ukatili, unyanyasaji, utelekezaji wa familia na majanga.
" Mafunzo haya yatanisaidia sana kuhakikisha nafikisha elimu Kwa jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza na jinsi gani ya kujikinga" Alisema Mtereko.
0 Comments