Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha mada kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia na mitandao ya kijamii kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) Mwanza.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Mamlaka ya Mwasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa imewanoa
wanafunzi wa elimu ya juu kuhusu matumizi sahihi ya maendeleo ya teknolojia
ikiwemo mitandao ya kijamii ili kuwaepusha na makosa yanayoweza kuwaingiza
kwenye migongano na mamlaka za usimamizi na utekelezaji wa sheria.
Akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Agustino (Saut) jijini Mwanza, Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa,
Francis Mihayo amewashauri vijana nchini kutumia maendeleo ya teknolojia kama
nyenzo ya kutanua wigo kujifunza na kujiendeleza kiuchumi badala ya mambo yanayokiuka sheria
ikiwemo kutuma ujumbe na picha zinazokiuka maadili na sheria.
“Sekta ya mawasiliano ni msingi mkuu wa ujenzi wa uchumi
duniani kwa sasa; nawasihi wanafunzi wa elimu ya juu kuitumia kwa manufaa yao
kielimu na kuichumi kupitia fani zao,” amesema Mihayo
Amesema kutokana na umuhimu wa maendeleo ya teknolojia, TCRA imekuwa ikitumia mikusanyiko ikiwemo taasisi za elimu ya juu kuelimisha umma, hasa vijana namna ya kutumia teknolojia kwa usahihi huku akiushukuru uongozi wa Saut kwa kutoa fursa kwa mamlaka hiyo kukutana na kuwaelimisha wanafunzi wa chuo hicho.
“Baadhi ya wanafunzi
wapya wanatoka maeneo na mazingira ambayo hawakuwa na matumizi makubwa ya
mitandao au walikuwa wanaitumia kwa usimamizi na uangalizi wa wazazi na walezi
wao; sasa wamefika chuoni ambako wanapaswa kujisimamia wenyewe, ndiyo maana
tunawapa msingi wa matumizi sahihi ya mitandao,” amesema Mihayo
Askari Polisi kutoka kitengo cha makosa ya mitandao, Musa
Zuberi amesema takwimu za makosa ya mitandaoni yanayoripotiwa polisi inaonyesha kuwa wanafunzi, hasa wa elimu ya
juu ni kati ya makundi ya kijamii yanayojikuta kwenye migogoro na mamlaka za
dola kwa matumizi mabaya ya mitandao.
“Kesi za picha zisizofaa na udhalilishaji kupitia mitandao ya
kijamii ni miongoni mwa makosa ya kimtandao yanayofanywa na baadhi ya wanafunzi
wa elimu ya juu; nawasihi kila mmoja atumie vema mitandao hii kuepuka mkono wa
dola,” amesema Zuberi
Fauzia Hashim, mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza Saut
ameishukuru TCRA kwa elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia ambayo itawawezesha
kuepuka makosa ya kimtandao.
0 Comments