Header Ads Widget

SENDIGA: JAMII YA RUKWA IMENUFAIKA NA MRADI WA LISHE ENDELEVU

Serikali imelipongeza Shirika la USAID/Lishe Endelevu kwa kutekeleza mradi wa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa lishe bora hatua iliyosaidia mkoa wa Rukwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa mwaka 2021/2022 katika utekelezaji mikataba wa lishe kati ya mikoa 26.


Pongezi hizo zimetolewa leo (Novemba 24, 2022) mjini Sumbawanga na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba katika ufunguzi wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajia kuisha mwaka 2023.


Akitaja mafanikio ya mradi huo, Waryuba alisema mradi wa Lishe Endelevu umesaidia halmashauri zote za Rukwa kwa sasa zinaweka bajeti katika afua za lishe na zinatoa pesa kutekeleza afua za lishe.


Mradi huo pia umetoa mafunzo kwa maafisa ugani ambao kwa kutumia stadi walizozifunza wameweza kuwajengea uwezo wakulima 13,416 jinsi ya kutumika mbinu bora za ufugaji na ukulima. 


Katika hatua nyingine Waryuba alitoa wito kwa Shirika hilo kufikiria kuendelea kubaki mkoani Rukwa ili kutokana na uhitaji wa elimu ya lishe bora kukabiliana na udumavu na kwenye jamii.


“Wito wetu kwenu wadau bado tunawahitaji mfikirie kuendelea kubaki mkoani Rukwa kutokana na uhitaji wetu katika kutekeleza masuala ya afua za lishe kwenye jamii “alisema Waryuba.



Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa USAD/Lishe Endelevu Dkt. Joyceline Kaganda alisema mradi umetekelezwa Rukwa kwa miaka minne tangu 2018 jamii imefanikiwa kuongeza ulaji wa vyakula vyenye protini kwa wingi ikiwemo samaki kupitia elimu ya ufugaji samaki kwenye mabwawa.. 


“Mradi unakwenda ukingoni lakini tunapigia debe wafadhili wasiondoke Rukwa na pia tunaomba serikali ichukue umiliki wa mradi huu baada ya Septemba 2023 ikiwemo kusimamia na kuwafuatilia maafisa ugani kutekeleza afua za lishe “alisema Dkt. Kaganda.


Kwa mujibu wa Dkt. Kaganda mradi wa Lishe Endelevu umefanikiwa pia kufikia vijiji zaidi ya 2000 katika mikoa minne iliyotekeleza mradi huo ambayo ni Rukwa, Morogoro, Dodoma na Iringa kwa kushirikiana na serikali kutekeleza afua za lishe.


Nao wawakilishi toka Wizara ya Kilimo Makoye Thobias na mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Wambura Messo walieleza kuwa serikali itaendelea kutoa miongozo kufanikisha agenda za lishe kwa ustawi wa wananchi.


Mradi wa Lishe Endelevu umelenga kuongeza juhudi za serikali katika kupambana na janga la udumavu kwa kuimarisha afya na lishe katika kundi la watoto wenye umri chini ya miaka mitano, vijana balehe na wakina mama walio katika umri wa kuzaa.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI