NA HADIJA OMARY LINDI
MKUU wa Mkoa wa Lindi Bi.Zainab Telack amewahasa Wanaume kujitokeza kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuacha tabia ya kutafsiri majibu ya vipimo vya wenza wao kuwa ndio majibu yao.
Rai hiyo imetolewa leo November 24/2022 na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack wakati wa ufunguzi wa wiki ya maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya ukimwi duniani katika viwanja vya Ilulu ambayo yanafanyika Mkoani humo.
Ndemanga alisema wanaume wamekuwa wazito kujitokeza kupima afya hususani virusi vya ukimwi kwani takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonyesha kuna kiwango cha chini cha upimaji wa virusi hivyo kwa wanaume ambapo ni sawa na asilimia 45.3 tu waliojitokeza ukilinganisha na wanawake ambao wamefikisha asilimia 55.9.
Ndemanga ameongeza kuwa hali hiyo ni hatari si kwa mtu binafsi bali hata kwa familia,kaya na Taifa kwa ujumla kwani inadhohofisha juhudi za serikali na wadau katika mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi hivyo ametaka watu watumie wiki hiyo ambayo huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali zitatolewa ikiwemo virusi vya ukimwi.
Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS),Dk. Leonard Maboko, amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya ukimwi kwa mwaka huu 2022 inayosema imarisha usawa inalenga katika kuangalia makundi ya watu walioachwa nyuma katika elimu ya upimaji wa Vvu ikiwemo kundi la wanaume ambao wanatajwa kuwa wapo nyuma kupima,kuanza dawa,kuendelea kunywa dawa huku kwa upande wa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo wakiwa wanaongoza.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi ambaye pia ni KatibuTawala Msaidizi-Utawala na Rasilimali Watu, Dkt. Bora Haule wakati anatoa salamu za Mkoa huo, alisema Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na wadau unaendelea kutoa huduma za kinga na tiba kwa waathirika wa virusi vya ukimwi kupitia vituo 130 vya kutolea huduma hizo vilivyopo kwenye Wilaya zote za Mkoa huo.
Alisema Katika lengo la walio na maambukizi kujitambua Mkoa huo umefikia asilimia 92,kwa walio na maambukizi kuwa katika matibabu asilimia 98 na wanaotumia dawa kushusha kiwango cha virusi mwilini umefikia asilimia 95.
Hata hivyo Dokta Bora pia alitumia nafasi hiyo,kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha mazingira kuwa rafiki kwa wadau mbalimbali wanaotekeleza afua mbalimbali za VVU na Ukimwi,upatikanaji wa dawa za ARV na vipimo vya kupima Vvu na wingi wa virusi kwani wakazi wa Mkoa wa Lindi ni wanufaika wa jitihada hizo.
0 Comments