Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Zaidi ya ekari 2000 zimeteketea kwa moto katika kijiji cha Itambo kata ya Idamba halmashauri ya wilaya Njombe moto uliowaka kwa siku tatu mfululizo na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha katika misitu ya watu binafsi na serikali.
Kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mwenyekiti wake Antony Mtaka Mkuu wa mkoa wa Njombe imefika kijijini humo na kushuhudia adha hiyo ambapo viongozi wa serikali ya kijiji hicho na kata akiwemo Sadick Mabena na Jimson Mwanza wamesema hadi sasa haijabainika chanzo cha moto huo licha ya kuzuka kwa mara ya sita katika vipindi tofauti.
Mhifadhi misitu Wilaya ya Njombe [TFS] Audatus Kashamakula amesema moto huo umeendelea kusababisha hasara kwa wananchi na serikali kwani katika kipindi cha miaka mitatu miti ya zaidi ya bilioni 400 imeteketea kwa moto.
Paulo Fugamila ni mkazi wa kijiji cha Itambo ambaye anasema wamekuwa wakiunguliwa na miti kijijini hapo lakini safari hii hasara imekuwa kubwa zaidi.
Afisa zimamoto Wilaya ya Njombe Loth Madauda anasema zoezi la uzimaji moto huo limekuwa gumu kutokana na ushirikiano duni toka kwa wananchi wenyewe kwani baadhi yao wamekuwa wakizima kwa kulipwa ujira na baadhi ya wenye mashamba hivyo kuwafanya wananchi kuwasusia wanaozima kwa kulipwa.
Kutokana na hasara hizo Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka anasema ipo haja ya kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na matukio ya moto kichaa huo unaoteketeza maelfu ya ekari za mashamba ya miti na kuwasababishia hasara kubwa wananchi na serikali.
Mtaka amesema miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kuitisha mikutano ya wawekezaji wote wa mashamba ya miti na kuwaorodhesha ili wawe wanatambulika na wafanyakazi wao wote wanaoshinda mashambani.
Kipindi hiki cha uandaaji mashamba,uchomaji mkaa pamoja na ulinaji asali kimekuwa kikisababisha majanga ya mengi ya moto mkoani Njombe yanayounguza mashamba ya miti.










0 Comments