Na Editha Karlo,Kasulu
MTANDAO wa mawasiliano ya jamii ya Tanzania(TZCNA)kwa kushirikiana na kituo cha Radio cha Buha FM Kasulu wamezindua kituo cha mawasiliano ya kidigitali kwaajili ya jamii ya Wilaya ya Kasulu ambacho kitatumiwa na wanachama wa mtandao pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Kigoma.
Akizindua chumba hicho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Kashushula alisema kuanzishwa kwa ushirika wa mitandao ya kijamii na huduma za kidigitali itachangia kuamsha ari ya jamii hasa wanaoishi vijijini kutumia tehama kama chanzo cha taarifa katika shughuli zao mbalimbali za maendeleo.
Kashushula alisema kuwa kutokana na mabadiliko ya kidigitali duniani kote sasa hivi matumizi ya tehama kwenye shughuli zote za kijamii hayakwepeki hivo chumba hicho kitakuwa ni chachu kwa wanakigoma wote kutumia zana za kisasa za mawasiliano.
‘’Niwapongeze kwa jambo hili nzuri la maendeleo kwaajili ya Wilaya yetu ya Kasulu na Mkoa kwa ujumla kwa kuzindua chumba hiki chenye kompyuta tano za kisasa zilizounganishwa kwaajili ya kuboresha na kuimarisha mfumo wa mawasilino kwa jamii watu wa Kigoma,Nina wahaidi kuwaongezea kompyuta zaidi katika kituo hiki cha mawasiliano ili kupanua wigo zaidi wa mawasiliano ya kiteknolojia’’Alisema
Awali Mtaalamu wa mawasiliano toka chuo kikuu cha dodoma Dk Jabela Matogolo wakati akitoa mada kwenye kongamano ameitaka jamii kutumia huduma za mawasiliano kujikwamua kiuchumi.
‘’Kuna pengo la asilimia 40 la wananchi kushindwa kutumia huduma za mawasiliano zilizopo kwenye maeneo yao,hivyo ni jukumu letu wanamtandao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutumia huduma za mawasiliano kidigital kwaajili ya maendeleo’’Alisema Matogolo
Mwenyekiti wa Kasulu Community Network Cooperativr Society,Siles Malli alisema watoto waliopo mashuleni wanapaswa kupewa elimu sahihi ya matumizi ya vifaa vya kidigitali ikiwemo kompyuta sambamba na kuvipata kwa gharama nafuu hii itawasaidia kupenda shule na kupunguza utoro.
Washiriki kutoka Mikoa ya Kigoma,Katavi,Dodoma,Ruvuma,Mara,Kagera na Dar es salaam wamehudhuria kongamano hilo la tatu la kitaifa la kujadili umuhimu wa matumizi ya internet kwa jamii na fursa za kiuchumi kupitia mitandao.







0 Comments